Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania ndio eneo maridhawa zaidi kwa utalii wa safari duniani

Tanzania ndio eneo maridhawa zaidi kwa utalii wa safari duniani

0 comment 33 views

Hatimaye baada ya mchuano mkali Tanzania imeibuka kuwa eneo linaloongoza zaidi duniani kwa utalii wa safari (hasa za kuona wanyama wa porini) ikiyashinda mataifa mbalimbali duniani ikiwemo nchi za Afrika.

Hii ni kwa mujibu wa Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) zilizotolewa usiku wa kuamkia Novemba 24, 2024 kisiwani Madeira, Ureno.

Zikitambulika kuwa sawa na “Tuzo za Oscars” katika tasnia ya utalii, World Travel Awards (WTA), ndio tuzo za juu zaidi duniani na tangu mwaka 1993, zimekuwa zikitambua mafanikio na umahiri katika ngazi ya mabara na kidunia katika kategoria anuai za utalii.

“Tunawashukuru wote waliotupigia kura kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiwemo wadau wa utalii na uhifadhi wenye hadhi ya kupiga kura lakini na mtu mmoja mmoja walioichagua Tanzania.

Tuzo hii ni ushahidi wa matokeo ya uhifadhi wetu mkubwa uliofanywa na viongozi wa awamu zote na unaoendelezwa katika Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia na uwekezaji mkubwa tunaoendelea nao katika kutangaza utalii kwani wengi walioipigia kura Tanzania maana yake ni wazi walitembelea na kuridhika na umaridhawa na uasili wa hifadhi zetu,” amesema Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyeongoza msafara kupokea Tuzo hiyo.

Awali mwezi Oktoba mwaka huu, Tanzania ilishinda Tuzo nne za WTA katika ngazi ya Bara la Afrika ikiwemo ile ya “Africa’s Leading Destination.

Awali katika Tuzo hizo kampuni binafsi inayofanya kazi Tanzania katika Hifadhi za Serengeti na Ruaha ya Serengeti Balloon Safaris nayo imeshinda Tuzo ya kuwa Kampuni Bora ya Baluni Duniani.

Baadhi ya nchi nyingine zilizoshinda ni Visiwa vya Saint Lucia (Honeymoon Destination), ugiriki (Athens, Leading City Destination), Ureno (World Leading Beach Destination), Ufaransa (Leading Events Destination), Peru (Cultural and Culinary Destination).

Nyingine ni Ureno (Praga, Emerging Tourism Destination), Hispania (Madrid, World Leading Meeting Destination) na Maldives (World Leading Destination).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter