Serikali imesema kuwa itaendela kushirikiana na Japan huku ikitoa wito kwa kampuni za Japan kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali katika sekta zenye maslahi ya nchi zote mbili ikiwa ni pamoja na kukuza uwekezaji binafsi.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma wakati wa Mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu Jenifa Christian Omolo kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alipokutana na kuzungumza na Naoki Yanase, Mkurugenzi Mkuu Kanda ya Afrika wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Omolo ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kutoa wataalamu wanaofanikisha kutekeleza miradi kwa wakati na kwa viwango vya juu na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania.
Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Japan ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Barabara ya Arusha-Holili, Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Maji Zanzibar Mjini, ujenzi wa barabara za mzunguko wa ndani katika jiji la Dodoma ambayo ipo katika utekelezaji.
‘’Tangu kuanzishwa kwa ushirikiano Mwaka 1960, Tanzania imenufaika kwa kiasi kikubwa na miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Japan na hivyo kuifanya Tanzania kuwa mnufaika mkubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara,’’ amesema Omolo.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya uchumi, Omolo amesema kuwa sera madhubuti za Serikali zimewezesha uchumi wa Tanzania kuendelea kuimarika ikirekodi kasi ya ukuaji wa asilimia 5.3 katika robo ya pili ya 2024, ikilinganishwa na 4.7 asilimia katika kipindi sawia cha mwaka 2023.
Aidha, mfumuko wa bei Oktoba 2024, ulifikia asilimia 3.0 ambayo ni ndani ya lengo na pia ni ndani ya wigo kwa mujibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) jambo lililochangiwa na sera nzuri za fedha, utoshelevu wa chakula na kudhibiti bei za bidhaa zinazotoka nje.