Home BIASHARAUWEKEZAJI Kampuni za Japan zakaribishwa Tanzania

Kampuni za Japan zakaribishwa Tanzania

0 comment 41 views

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa Kampuni za Japan kuwekeza nchini Tanzania ili kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali za uzalishaji kwa faida ya pande zote mbili.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma wakati akiagana na Balozi wa Japan nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Yasushi Misawa ambapo pamoja na mambo mengine amemhakikishia pia Balozi huyo kuwa Tanzania na Japan zitaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na kijamii kwa faida ya nchi hizo mbili.

Amesisitiza kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji ikiwemo sekta ya kilimo itakayoiwezesha Tanzania kuwa ghala la chakula lakini pia uwekezaji katika miundombinu ikiwemo uendeshaji wa Reli ya Kisasa ya SGR.

Aidha, katika mazungumzo yao, Dkt. Nchemba ameishukuru Japan kwa uwekezaji mkubwa uliochangia maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na nchi hiyo katika sekta za kilimo, afya, nishati, na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara ya mzunguko katika jiji la Dodoma.

“Katika kipindi chako pekee, tumeshuhudia Tanzania na Japan zikisaini mikataba ya mikopo nafuu yenye thamani ya yen ya Japan bilioni 10 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 151 pamoja na msaada wa yen bilioni 5.5, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 83. Tunakushukuru sana na tunakuomba uendelee kuwa Balozi mzuri wa Tanzania hata baada ya kumaliza muda wako,” amesisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Balozi Misawa, aliyeambatana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Ara Hitoshi, amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na nchi yake umedumu kwa zaidi ya miaka 60 ambapo katika kipindi hicho, Japan imesaidia utekelezaji wa zaidi ya miradi 360 ya kijamii na kiuchumi.

Amebainisha kuwa baadhi ya miradi hiyo iko katika sekta ya nishati ukiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga, ujenzi wa mradi wa umeme unaounganisha Tanzania na Kenya pamoja na mpango unaoendelea kati ya Tanzania na Japan kupitia Wizara ya Nishati wa kujenga mradi wa umeme wa joto ardhi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter