Waziri wa Madini Anthony Mavunde amezindua rasmi shughuli za uchimbaji madini katika mgodi wa Porcupine North- uliopo Makongorosi Wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya.
Mgodi huo unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited umezinduliwa Aprili 03, 2025.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi Waziri Mavunde amesema kuwa hatua hiyo ni matunda ya uamuzi wa Serikali kurudisha leseni ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha unawekwa utaratibu mzuri wa kuongeza mapato ya nchi kupitia sekta ya madini.
“Eneo hili ni eneo ambalo leseni hodhi zimerudi serikalini kwa mujibu wa sheria. Baada ya kumalizika shauri la kimahakama na mwekezaji wa awali, serikali iliweka utaratibu wa wazi kumpata mwekezaji atakayeendesha eneo hili la uchimbaji.
Kampuni ya Shanta Gold Mining Limited ilishinda kwa masharti ya kuanza uchimbaji ndani ya miezi 18, ambapo mashapo yaliyothibitishwa kwa sasa yanafikia wakia 110,000 na upo uwezekano baada ya utafiti zaidi kufikisha mashapo ya wakia 400,000 ambazo kupitia mrabaha, kodi na tozo mbalimbali zitasaidia kuongeza makusanyo ya Serikali,” amesema Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde amesema kuwa leseni moja iliyokuwa katika eneo la Saza, Mkoa wa Songwe, imekabidhi kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kundi hilo linanufaika na rasilimali za madini.
Eneo hilo la Saza lililokabidhiwa kwa wachimbaji wadogo, linakadiriwa kuwa na mashapo ya dhahabu yenye wakia laki mbili, thamani yake ikiwa ni takriban shilingi trilioni 1.2 kwa bei ya sasa ya dhahabu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema tukio la uzinduzi wa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo ni ushuhuda wa mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini chini ya uongozi na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake na kwamba mgodi huo utakuwa mfano wa kipekee hapa nchini.
Mgodi huu pia utatoa fursa za ajira kwa Watanzania, kuchangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).