Mkurugenzi wa sensa na takwimu za jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo ameeleza kuwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Machi umepungua na kufikia asilimia 3.9 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwezi Februari mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Kwesigabo amesema kuwa bidhaa za vyakula kama vile mtama, unga wa muhogo, maharage, mihogo mibichi na ndizi zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupungua kwa mfumuko wa bei huku akifafanua kuwa, hali hiyo inaashiria kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma imepungua tofauti na ilivyokuwa mwezi Februari.
Mbali na hayo, Mkurugenzi huyo pia amezungumzia hali ilivyo katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na kusema kuwa mfumuko wa bei nchini Uganda umepungua kutoka asilimia 2.1 mwezi Februari hadi asilimia 2.0 mwezi Machi wakati nchini Kenya imepungua kutoka asilimia 4.46 mwezi Februari hadi asilimia 4.18 mwezi Machi.