Home BIASHARA Tukuze vipaji, ni ajira

Tukuze vipaji, ni ajira

0 comment 145 views

Mara nyingi watu wengi hutegemea tu elimu kuwa ndio mkombozi pekee katika maisha. Ni kweli kuwa huwezi kufika mbali na kuendelea bila ya kuwa na elimu. Lakini umeshawahi kufikiria kuhusu kipaji ulichonacho? Kuendeleza kipaji chako sio njia moja wapo ya kujiajiri au kuajiriwa? Ni watu wangapi hapa nchini hupata fursa ya kukuza vipaji vyao na kujiendeleza kiuchumi?

Katika jamii zetu, wazazi wengi huwa hawaangalii sana vipaji vya watoto wao. Wengi huona kama sio kitu ambacho kinampatia mtu fursa na kumjengea ajira rasmi. Wazazi wengi hupambana watoto wao wapate elimu na kufanya hivyo wakati wengine kunaua kipaji ambavyo kama vingeendelezwa, vingeweza kuwa chanzo cha ajira na kipato kizuri tu. Mifumo yetu ya elimu nayo haijaweka mkazo wa kutosha katika kukuza vipaji vya wanafunzi na kuwafungulia milango ili waone kuwa navyo pia vinaweza kuwa ajira yao.

Ni muhimu kujiuliza kuwa kwanini watu wengi huona kama kukuza kipaji cha mtoto sio jambo jema? Kwani hakuna mifano hai ya watu ambao waliamini katika vipaji vyao na wakaendelea? Ni kwanini asilimia kubwa ya wazazi huona kama sanaa ni uhuni na si ajira rasmi kama zilivyo ajira nyingine? Watoto wenye vipaji waviache tu vipotee bila kuvitumia?

Ni dhahiri kuwa lazima hatua zichukuliwe ili kuondokana na dhana ya kwamba maendeleo hayawezi kupatikana kutokana na kipaji cha mtu. Kama wazazi ama walezi wote wangefikiria hivyo basi kusingekuwa na wachoraji, wachongaji vinyago, waigizaji na hata wanamuziki kote hapa nchini. Sanaa ni sekta muhimu katika maendeleo kama zilivyo hizo nyingine lakini mara nyingi huwa haipewi kipaumbele.

Kupitia shughuli za kisanaa kama vile muziki, uigizaji na hata uchoraji watu wameweza kujiajiri na wengine wameenda mbali zaidi hadi kufungua makampuni yao binafsi na kutoa ajira kwa wengine. Hakuna anayekataa kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na ni muhimu kusoma na kufikia malengo yako lakini wakati unafanya hivyo, kama una kipaji na unaamini unaweza kufika nacho mbali ni vizuri kukiendeleza na kuona ni wapi kitakupeleka.

Vijana nao wanatakiwa kujiamini kutumia vipaji vyao kujiajiri na kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali ili kupiga vita tatizo la ajira lililopo kote hapa nchini. Kwa kujiajiri na kuweza kujiiingizia kipato, pia wanapata nafasi ya kuchangia katika pato la taifa. Ni muhimu kuonyesha juhudi na nia ya kufanikiwa ili hata wale ambao hawakuwa na imani kuwa vipaji vinaweza kutumika kujiajiri waone kuwa inawezekana.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter