Mkurugenzi wa Taasisi ya New Vision Consortium (NVCT) Pily Khamis Lapda ametoa wito kwa wanawake wa visiwani Zanzibar kutumia vizuri fursa ya ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kufanikiwa kujiajiri. Lapda ameeleza kuwa asilimia kubwa ya wanawake wamekuwa wakifanya shughuli za ujasiriamali kwa mazoea na hivyo kushindwa kufikia malengo yao.
Amesema kuwa kuna njia mbalimbali za kuwakomboa wanawake na ameshauri wanawake nchini kujiamini na kujiwekea malengo ya kudumu ya biashara ambayo yawasaidia kumiliki mitaji mikubwa ya kibiashara.
Taasisi ya NVCT imekuwa ikisimamia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kitaalamu makundi mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha kuwa na uwezo wa kutumia fursa mbalimbali za ujasiriamali ili kuleta maendeleo. Mkurugenzi huyo amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kujifunza mbinu za kujikwamua kiuchumi na kuwa wabunifu ili kukuza biashara zao.