Baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro kukamata bidhaa mbalimbali ambazo zimeingizwa nchini pasipo wafanyabiashara kufuata kanuni na taratibu, mamlaka hiyo imeteketeza bidhaa hizo zenye thamani ya takribani Sh. 23 milioni. Akizungumzia tukio hilo, Meneja Msaidizi Forodha mkoani humo Godfrey Kitundu amesema baadhi ya bidhaa zilizoteketezwa tayari zilikuwa zimeisha muda wake wa matumizi kwa ajili ya binadamu.
Ametaja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na mafuta ya kupikia, vipodozi, vifaa tiba na kemikali za hospitali.
Kwa upande wake, mkaguzi kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) mpakani Holili Edward Mwamilao ameeleza kuwa bidhaa hizo zingeweza kuleta athari kubwa endapo zingeingizwa sokoni.