Zaidi ya makampuni arobaini (40) kutoka nchi nane duniani yanatarajiwa kushiriki katika maonyesho makubwa ya bidhaa za maziwa yanayoanza leo jijini Arusha huku unywaji wa maziwa kwa watanzania ukionekana kuwa chini tofauti na takwimu kutoka nchi nyingine. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya maziwa nchini Charles Malunde alipokuwa katika kikao cha utangulizi kuelekea maadhimisho ya wiki ya unywaji wa maziwa.
Akizungumzia maonyesho hayo, Mkurugenzi wa sera, utetezi na mipango kutoka Baraza la kilimo Tanzania Timoth Mbaga amewataka wadau kujitokeza kwa wingi kwani maonyesho hayo yanalenga kuwawezesha wafugaji kupata elimu na kufahamu teknolojia za kisasa za ufugaji . Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Arusha Gabriel Daqqaro amesema serikali inashirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuwezesha uwekezaji wa kisasa wa sekta ya mifugo.
Maonyesho hayo yanafanyika kitaifa jijini Arusha kuanzia leo hadi Juni 01 katika viwanja vya Themi na yatafunguliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhanga Mpina na kufungwa na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo.