Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa taasisi ya Repoa Dk. Abel Kinyondo amesema ili kuwavutia zaidi wawekezaji na wafanyabiashara, serikali inatakiwa kuboresha mazingira ya biashara kwa kupunguza wingi wa kodi kwani kufanya hivyo kutaimarisha vyanzo vyake vya mapato pamoja na kufanikisha utekelezaji wa bajeti.
Dk. Kinyondo ameeleza kuwa mazingira rafiki zaidi yanahitajika ili kujenga imani kwa wawekezaji ambao kwa kiasi kikubwa wanachangia ongezeko la ajira na kuongeza vyanzo vya mapato. Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, kuendelea kuwatoza kodi wajasiriamali wachache walioitikia wito na kujisajili kunawatia hofu baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini.
Dk. Kinyondo amesema japokuwa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) imekuwa na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuongeza wigo wa makusanyo ya mapato, mazingira mazuri zaidi yanapaswa kutengenezwa na serikali ili kuwatoa hofu wawekezaji na kukaribisha watu wengi zaidi kufika nchini kwa lengo la kuwekeza.