Shirika la usafiri wa anga la Etihad limetangaza kusitisha rasmi safari zake kati ya Abu Dhabi na Dar es salaam kuanzia Oktoba mwaka huu. Shirika hilo limefikia uamuzi huo baada ya kupata hasara kwa miaka miwili mfululizo hali iliyowalazimu kupanga upya mikakati yao ya kiutendaji na uwekezaji.
Mkakati wa kupitia upya safari za shirika hilo la ndege ni sehemu moja wapo ya kuboresha biashara baada ya kupitia kipindi kirefu cha kupata hasara.
Abiri waliokuwa wakitumia usafiri huo sasa watalazimika kuchukua ndege za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) hadi Nairobi na kisha kuunganishwa na shirika hilo mpaka Abu Dhabi.
Shirika la Etihad lilifungua rasmi safari za kuja Tanzania Desemba 2015 ikiwa ni kituo cha tatu ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Nairobi (Kenya) na Entebbe (Uganda).
Mwaka jana, Etihad ilisitisha safari zake mbalimbali za Entebbe, Jaipur, San Francisco na Venice kutokana na mkakati mpya.