Mwenyekiti wa Mfuko wa Maendeleo ya Sukari nchini Deo Lyatto amesema japokuwa ushuru wa sukari umepanda na kufikia asilimia 35 kutoka asilimia 25 ya hapo awali, bei yake imeendelea kuwa nafuu ikilinganishwa na nchi nyingine.
Lyato amesema hayo katika mkutano wa nane wa wadau wa sukari ulioandaliwa na mfuko huo kwa kushirikiana na Bodi ya Sukari mkoani Morogoro.
Mbali na hayo, Lyato pia amechukua fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa sukari inayozalishwa hapa nchini inakidhi vigezo na inadhibitishwa na mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA).
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama vya Wakulima wa Miwa (Tasga) Dk. George Mlingwa ametoa wito kwa serikali kusitisha uagizaji wa sukari kutoka nje ili kunusuru viwanda vya ndani. Amedai kuwa viwanda vya ndani vitashindwa kukua na kujiendesha kama sukari kutoka nje itaendelea kuletwa na kuuzwa nchini kwa bei rahisi.