Baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kupiga marufuku wanunuzi wa kahawa kuwafuata wanakijiji na badala yake kahawa iuzwe kwa njia ya mnada, Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imefanya mnada kwa mara ya kwanza tangu Waziri Mkuu kutoa agizo hilo.
Katika mnada huo, kahawa aina ya Arabika imeuzwa kati ya Dola za Marekani 115 na 122.20 kwa gunia la kilo 60 wakati kahawa ya Robusta yenyewe ikiuzwa kati ya Dola 79.20 na 79.40 kwa gunia moja. Mnada huo pia umeweka sokoni kahawa iliyosalia katika msimu wa mwaka 2017/2018 pamoja na mpya iliyoingizwa sokoni na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU).
Kwa upande wake, Dalali Mkuu wa mnada huo Desderi Mboya amesema KCU imewasilisha takribani magunia 1,991 ya kahawa. Naye Meneja Mauzo wa Nje wa KCU Josephat Sylvand ameeleza kuwa KCU imefanikiwa kukidhi viwango vya ubora wa kahawa inayohitajika kutokana na kuwepo kwa mradi wa kuzalisha kwa njia ya kilimo hai.
Mwanzoni mwaka huu, Waziri Mkuu alipiga marufuku wanunuzi kuwafuata wanakijiji moja kwa moja na kuagiza kahawa iuzwe kwa njia ya mnada na kuzuia utoaji wa vibali kwa wanunuzi.