Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) kwa jitihada kubwa wanayofanya katika kujenga mitambo ya maji ambayo imeongeza upatikanaji wa maji kutoka lita milioni 300 ya hapo awali hadi kufikia lita milioni 502 kwa siku. Prof. Mbarawa ameitaka mamlaka hiyo kuongeza juhudi na kukamilisha usambazaji maji kwa kuwasimamia wakandarasi wanaohusika na mradi huo kwa karibu ili kuhakikisha ujenzi huo wa miundombinu unafanikiwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Mbali na kuipongeza DAWASA, Waziri huyo ameiagiza mamlaka hiyo kuangalia namna ya kudhibiti maji yanayozalishwa kwani takribani nusu ya lita milioni 502 hupotea kila siku kutokana na watu wasio waaminifu kuiba maji hayo. Prof. Mbarawa ameagiza mamlaka hiyo kuboresha huduma ili kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi na salama.