Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji ameshauri wafanyabiashara mkoani Kigoma kutokubali kulipa kodi kwa makadirio ikiwa wataalamu wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawajafika na kutathmini biashara zao. Dk Kijaju amesema hayo katika mkutano wake na wafanyabiashara na kuongeza kuwa, ni lazima kuwe na uhalisia katika ulipaji mapato kulingana na biashara husika
“Zipo biashara zinazokuwa lakini pia zipo biashara ambazo zilipata changamoto hivyo mtaji wake kupungua ni lazima watumishi wa TRA wataalamu wa masuala ya kodi wakatembelea biashara husika wakakagua vitabu kwa uhalisia wake ndipo wakadirie kodi anayopaswa kutozwa mfanyabiashara husika”. Amefafanua Dk. Kijaji.
Mbali na hayo, Naibu Waziri huyo amewataka wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki (EFD) ili walipe mapato kulingana na biashara wanayofanya. Vilevile,ameitaka TRA kutoa mafunzo na semina kwa wafanyabiashara kuhusu namna ya kulipa kodi ili walipe kodi kwa hiari.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara mkoani Kigoma, Raymond Ndabiyegese amesema utendaji kazi wa baadhi ya watumishi wa TRA mkoani humo umefanya pande hizo mbili kutoelewana kutokana na kufunga maduka bila mamlaka hiyo kufanya mazungumzo na wafanyabiashara.