Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amebainisha kuwa Tanzania bado inahitaji wawekezaji wakubwa kwenye viwanda vya mazao ya kilimo, mifugo na samaki kutoka China. Waziri Mkuu amesema hayo alipokutana na kuzungumza na Waziri wa Kilimo wa China, Han Changfu, jijini Beijing ambapo amesisitiza kuhusu mataifa hayo mawili kushirikiana hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania imeweka nia ya kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.
“China ni rafiki yetu na pia imepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya viwanda, hivyo tunahitaji kuendelea kushirikiana nayo ili tuweze kupata na teknolojia sahihi ya viwanda mbalimbali”. Ameeleza Majaliwa.
Waziri Mkuu pia amechukua nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka China kufika Tanzania na Zanzibar akisema watapatiwa ardhi ya kujenga viwanda ambavyo vitatumia mazao ya kilimo, mifugo na bahari, hususani samaki, ambayo mengi yanapatikana nchini kwa wingi. Vilevile, Waziri Majaliwa amesisitiza Tanzania inahitaji soko la uhakika la mbaazi na soya nchini China, ili kuwawezesha wakulima wa mazao hayo.
“Tumelazimika kutafuta masoko ya mazao hayo hapa China ili kutowakatisha tamaa wakulima wetu, kwani itakuwa vigumu kwao kuendelea kulima mazao hayo kwa wingi bila ya kuwa na uhakika wa soko”. Amesema Majaliwa.
Kwa upande wake, Waziri Changfu wa China amesema nchi hiyo ipo tayari kutoa mafunzo na kuwaelimisha watanzania kwa kuandaa semina zitakazowawezesha washiriki kuongeza ujuzi wao na hivyo kupelekea maofisa ugani kufanya kazi kwa ustadi zaidi.