Home KILIMOKILIMO BIASHARA Mbinu bora za kulima alizeti

Mbinu bora za kulima alizeti

0 comment 154 views

Alizeti ni moja kati ya mazao ya biashara yenye uhitaji mkubwa kwa maisha ya binadamu. Hii inatokana na wananchi wengi wa Tanzania kutumia malighafi ya zao hili ikiwemo mafuta ya kupikia na mashudu (makapi) yanayopatikana baada ya uzalishaji wa mafuta. Mashudu yamekuwa yakitumika kama chakula kwa ajili ya mifugo mbalimbali ikiwemo nguruwe na ng’ombe.

Kanda ya kati hasa mkoa wa Singida ni wazalishaji wakuu wa alizeti na hivyo zao hilo limefungua fursa nyingi za kibiashara mkoani humo ikiwemo viwanda na fursa za kiuchumi na usafirishaji. Pamoja na zao hili kuwa na uhitaji mkubwa bado uzalishaji wake umekuwa ukipungua, hii inatokana na kutotiliwa mkazo kwa zao hili hasa katika kutafuta mbinu za upanuaji soko la nje pamoja na uwepo wa mazao mengine yenye kuzalisha mafuta ikiwemo pamba na mkichikichi.

Yafuatayo ni mawazo ya kuanzisha kilimo cha alizeti kwa wakulima wadogo na wakubwa na namna unavyoweza kujihakikishia faida kubwa kupitia zao hilo.

  1. Jifunze kwa kina kuhusu alizeti. Hii ni mbinu ya kwanza itakayokusaidia kuwa na uhakika wa kile unachotaka kukianzisha. Jaribu kufanya utafiti wa soko, mbinu za uzalishaj pamoja na vifaa vinavyohitajika. Hii inaweza kufanyika kupitia vitabu vya kilimo pamoja na kuperuzi mitandaoni.
  2. Jifunze kuhusu aina za mbegu na suala la hali ya hewa. Kufahamu aina ya mbegu inayofaa kulingana na mazingira unayotaka kuanzisha kilimo cha alizeti ni jambo la muhimu. Kujua kama aina ya udongo uliopo katika maeneo hayo pia unafaa kulingana na mbegu ya aina fulani itakusaidia kupata mavuno mazuri na yenye kuridhisha.
  3. Andaa rasilimali na vitendea kazi ikiwemo zana za kilimo. Rasilimali, ikiwemo mbegu, zana za uzalishaji zitategemea kilimo unachotaka kufanya. Kama ni kiwango kikubwa basi zana kubwa pia ikiwemo trekta,mbegu za kutosha zinahitajika. Hivyo ni vyema kuandaa rasilimali zinazoendana na aina ya kilimo unachotaka kuanzisha.
  4. Andaa Ardhi. Baada ya kuwa umeandaa vitendea kazi suala linalofuata ni kununua ardhi au kukodi. Itahitaji pesa kununua pamoja na kuliandaa shamba kwa ajili ya kilimo
  5. Nguvu kazi na waajiriwa. Kama umeanzisha kilimo kwa kiwango kikubwa ni vyema kuwaajiri wataalamu wenye ujuzi wa kutosha. Hii itasaidia kuepukana na gharama za kutafuta wataalamu toka sehemu mbalimbali lakini pia itasaidia kutatua matatizo na changamoto zinazoweza kupelekea kilimo chako kukwama.
  6. Maji ya uhakika. Kilimo cha alizeti kinahitaji mvua au maji ya kadri. Ni vyema kujua mazingira unayotaka kuanzisha kilimo hicho kama yana mvua za kutosha na kama hakuna mvua basi uwepo wa maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji. Uwepo wa mabwawa, mito na matanki ya maji yatahakikishia mimea uwepo wa virutubisho vya kutosha.
  7. Chukua tahadhari. Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kulinda alizeti. Zao la alizeti linashambuliwa na wadudu pamoja na ndege hasa kipindi ambacho mbegu zake zinaanza kukomaa. Zipo njia za asili na za kisasa ambazo zimekuwa zikitumika kuzuia ndege waharibifu wa zao hilo ikiwemo kuchonga vinyago, kutega mitego ya kuwanasa kama ulimbo.
  8. Soko. Mkulima anashauriwa kutafuta soko pindi mazao yanapokomaa. Kama kutakuwa mabadiliko basi mkulima anashauriwa kutafuta soko sehemu nyingine.

Kilimo cha alizeti ni zao linalolipa endapo mkulima ameweka nia madhubuti katika kuwekeza kwenye kilimo hicho. Uzalishaji wa mazao bora ni moja kati ya vitu vinavyochochea wafanyabiashara wa zao hilo kutamani kufanya biashara na wewe.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter