Home VIWANDAUZALISHAJI Jinsi wazawa wanavyoweza kushiriki katika miradi mikubwa ya serikali

Jinsi wazawa wanavyoweza kushiriki katika miradi mikubwa ya serikali

0 comment 99 views

Tangu kuingia kwa serikali ya awamu ya tano chini ya Dk. John Pombe Magufuli kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa hasa ya ujenzi imeshamiri kwa kasi ambayo haikutarajiwa na watu wengi ndani na nje ya Tanzania. Miradi hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kwa kutumia vyanzo vya fedha kutoka ndani na nje, imekuwa ikivutia wawekezaji kutoka mabara ya Ulaya na Asia kuja kuwekeza na kupigania kupata tenda mbalimbali katika miradi hiyo.

Miradi kama ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja nchini kupitia mkoa wa Tanga, ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge),ujenzi wa mradi wa umeme wa Stieglers Gorge na ule wa Kinyerezi imekuwa ikivutia kampuni za nje ya nchi kuja kutafuta tenda za kutoa huduma mbalimbali hali inayowatia shaka watanzania ambao kwa muda mrefu wamekua wakililia kupata nafasi hizo.

Ushirikishwaji wa watanzania katika miradi hii (Local Content Inclusion) imekuwa mjadala katika makongamano mengi likiwemo lililofanyika wiki hii la mafuta na gesi ambalo lilihudhuriwa na watu 340 kutoka mabara tofauti yakiwemo makampuni yenye uzoefu katika miradi ya uchimbaji wa mafuta na gesi duniani. Kongamano hilo lililozinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulika na Mazingira January Makamba lilielekeza maeneo mbalimbali ambayo watanzania wanaweza kushirikishwa katika miradi hiyo na maeneo yafuatayo yaliainishwa.

HISA

Kutokana na makampuni mengi Tanzania kutokuwa na uzoefu na miradi mikubwa hasa ya uchimbaji wa mafuta na gesi imeshauriwa ili kuweka ushirikishwaji wa watanzania katika miradi hii ni vyema watanzania wakashirikiana na wageni kupitia ununuaji wa hisa katika makampuni hayo ili wajenge uzoefu na ujuzi wa usimamizi wa miradi hii kabla ya kupewa tenda. Akichangia kuhusu suala hili Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema suala la umiliki wa hisa kwa watanzania katika makampuni hayo lazima hisa hizo zianzie 25% kwenda juu na suala hili lipo kisera na kisheria.

BIMA

Hili ni eneo lingine ambalo litaongeza ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hii mikubwa nchini. Makampuni yatakayoshinda tenda katika miradi hii lazima yakate bima mbalimbali kama za afya, ujenzi na usafiri. Hivyo imeshauriwa kampuni za ndani kuangalia kwa umakini fursa hii muhimu kwani hakuna mradi ambao utakidhi vigezo pasipo kuwa na bima.

USAFIRI

Ujenzi wa miradi hii huchukua muda fulani japo ni kipindi kirefu hivyo kampuni nyingi hutegemea kampuni za ndani katika kutoa baadhi ya huduma ili kuepusha kupata hasara hasa baada mradi kuisha. Usafiri ni moja ya eneo ambalo huitaji kampuni za ndani kuwekeza na kushirikiana na waendesha mradi. Huduma kama za kukata tiketi za ndege, magari ya kutembelea, madereva, gereji na vingine vinawategemea sana wazawa ili kuongeza ili kwenda vizuri.

CHAKULA NA MALAZI

Wawekezaji wakubwa baadhi huja na timu nzima ya wataalamu ambao wanakuwa wanahitajika kwa kipindi fulani hivyo ni vigumu kuwa na malazi ya kudumu pamoja na dhana za kupikia na huduma nyingine zinahusiana na hizo. Wazawa hupewa nafasi hii ya kuhudumu kwa malazi na chakula kwa kipindi chote ambacho wataalamu hawa watakachokuwepo. Ili kupata nafasi hii, mzawa anapaswa kuwa leseni muhimu za biashara kutoka mamlaka mbalimbali zinazohusika pamoja na mtaji wa uhakika.

AFYA NA USALAMA

Pengine sekta hii ni muhimu kuliko zote zilizoanishwa. Afya bora ni muhimu kwa rasilimali watu ili kuleta utendaji wenye tija. Miradi hii hushirikisha watu wa taaluma mbalimbali wakiwemo mafundi mitambo na wakandarasi ambao wanahitaji vifaa vya kujikinga na ajali kazini (Safety Equipments) maana kundi hili lipo hatarani kupata majeraha na maradhi kulingana na asili ya kazi yenyewe. Hii ni sekta ambayo wazawa wanatakiwa waipiganie ipasavyo na wakiipata waitendee haki ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hii.

BENKI

Hii ni sekta mama katika kujenga uchumi wa nchi hasa hususani wakati wa miradi mikubwa. Benki za ndani lazima zipewe kipaumbele katika mchakato wa ujenzi wa miradi hii. Makampuni kutoka nje huja na mitaji ambayo huhifadhiwa katika benki za ndani ili kurahisisha malipo mbalimbali katika ujenzi. Benki ni eneo zuri la ushirikishwaji wananchi hasa katika kupitisha malipo ya wafanyakazi ambao watakuwa na wigo mpana wa kupata huduma. Huduma kama mikopo kwa wafanyakazi wenye mikataba na wajasiriamali wanaozunguka eneo husika ni sehemu mojawapo ya ushirikishwaji wananchi.

MAHUSIANO YA JAMII NA RASILIMALI WATU

Kampuni inahitaji kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka ili kurahisisha utendaji kazi wake hasa shughuli za kila siku. Mahusiano haya hujengwa kwa ushirikiano kati ya makampuni, wafanyakazi, serikali na vyombo vya habari. Kupitia miradi hii mikubwa wazawa wanaweza kushirikishwa katika maeneo haya hasa ikizingatiwa kampuni huitaji idadi kubwa ya wafanyakazi wa muda mfupi na wasio na ujuzi wa kutosha hivyo lazima washirikiane na wazawa.

Licha ya hamasa mbalimbali ambazo serikali na wadau wa mafuta na gesi kama PURA, EWURA, TANESCO, TPDC, TPA, TRA na wengine wamekuwa wakitoa kwa wazawa ili kuongeza ushirikishwaji wao hasa kwa sekta binafsi, watanzania wanapaswa kuamka na kuanza kupigania fursa hizi ambazo hugharimu fedha nyingi kwa mfano mradi wa gesi (LNG) ambao utagharimu kiasi Dola za Marekani Bilioni 30.

Abdulsamad Abdulrahim ambaye ni Muandaaji wa kongamano la mafuta na gesi kuhusu uamkaji na ushirikishwaji wa wananchi alisema, “Serikali imeshaweka Sheria ya 25% sasa ikifika wakati mtanzania ukipewa nafasi lazima uitumie vizuri” . Kuhusu suala la wazawa kushindwa tenda katika hatua za awali alisema, “Inatakiwa wazawa wakiomba tenda wapewe feedback (mrejesho) ili kama wameshindwa wajue walipokosea ili wajirekebishe watapoomba tena”.

Kongamano la mafuta na gesi licha ya uchanga wake limekuwa na mafanikio makubwa ndani ya miaka miwili toka lianzishwe ambapo limefanikiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa mafuta na gesi kuanzia wawekezaji, wachimbaji, watafiti, serikali, sekta binafsi na nchi ambazo miradi hii imeshafanyika kama Tridad&Tobago, Uingereza na New Guinea.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter