Home BIASHARA Mfumuko wa bei wapanda

Mfumuko wa bei wapanda

0 comment 93 views

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo ametangaza kuwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia Septemba 2018 umeongezeka na kufikia asilimia 3.4 kutoka asilimia 3.3 ya mwaka ulioishia mwezi Agosti. Kwesigabo amewaambia waandishi wa habari kuwa hali hiyo inaashiria kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Septemba 2018 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi uliopita.

Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Septemba 2018 kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kinachoishia mwezi Septemba 2018 zikilinganishwa na Septemba 2017. Baadhi ya bidhaa zisizo za chakula ambazo zimepelekea kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na vileo na bidhaa za tumbaku (asilimia 1.9), nguo na viatu (asilimia 3.2), vifaa vya matengenezo na ukarabati wa nyumba (asilimia 5.2), mafuta ya taa (asilimia 18.7), mkaa (asilimia 11.2), gharama za kumuona daktari hospitali za binafsi (asilimia 5.5), dizeli (asilimia 19.9) na petrol (asilimia 15.8).

Kwa upande wa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba nchini Kenya umeongezeka hadi kufikia asilimia 5.70 kutoka asilimia 4.04 kwa mwaka ulioishia Agosti 2018 huku nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2018 umepungua hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti 2018.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter