Home KILIMO Serikali yaipa NFRA Bil 15 ununuzi wa nafaka kukabiliana na upungufu wa chakula yanapotokea majanga

Serikali yaipa NFRA Bil 15 ununuzi wa nafaka kukabiliana na upungufu wa chakula yanapotokea majanga

0 comment 99 views

Na Mathias Canal-WK, Tunduma-Mbeya

Katika kukabiliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza pindi nchi itakapokuwa kwenye majanga, Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 15.0 za kitanzania kwa ajili ya ununuzi wa mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi Chakula (NFRA) katika mwaka wa fedha 2018/2019.

Tayari Wakala wa Taifa wa Hifadhi Chakula (NFRA) umeanza msimu wa ununuzi tangu mwezi Agosti 2018 ambapo nafaka wanayonunua ni kutoka kwa wakulima na vikundi vya wakulima kote nchini.

Waziri wa Kilimo Dkt Charles Tizeba (Mb), amebainisha hayo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani Kitaifa ambayo yamefanyika kwenye viwanja vya JK Nyerere katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

Vilevile, NFRA inaendelea kuboresha uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kwa kuimarisha kanda zake kupitia mradi wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kisasa ili Kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka.

Dkt Tizeba alisema kuwa Kupitia mradi huo miundombinu ya kisasa ya hifadhi ya chakula zikiwemo maghala na vihenge vya kisasa vinajengwa katika Halmashauri za Wilaya za Babati (Tani 40,000), Mpanda (Tani 25,000) , Sumbawanga (Tani 40,000), Mbozi (Tani 20,000), Songea (Tani 50,000), Shinyanga (Tani 35,000), Dodoma (Tani 20,000) na Makambako (Tani 30,000).

Alisema, Hifadhi hizo zitatumia teknolojia ya kisasa ya kuhifadhi mazao na hivyo kupunguza upotevu wa mazao ghalani kwa kiasi kikubwa. Aliongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha NFRA kuongeza uwezo wake wa kuhifadhi nafaka kutoka Tani 251,000 hadi kufikia Tani 501,000 ifikapo mwaka 2019/2020.

MWISHO.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter