Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ametoa Sh. 20 milioni katika harakati za kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi wa Nyamazobe wilayani Nyamagana mkoani Mwanza waliojitolea kujenga barabara yenye urefu wa kilomita moja ambayo inakadiriwa kuwezesha kaya 900 na wananchi takribani 3,005 kujiimarisha kiuchumi pindi itakapokamilika.
Akikabidhi fedha hizo kwa niaba ya Rais Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Seleman Jafo amewaambia wananchi kuwa, Rais amefurahishwa na uzalendo uliochukuliwa na wananchi hao kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha mawe.
“Rais amesema ninyi ni wananchi wa kupigiwa mfano na alivyofurahi amenikabidhi kiasi cha Shilingi Milioni 20 niwaletee ili ziwaongezee nguvu kwenye ujenzi huu wa barabara mlioanza. Rais amesisitiza kuwa fedha hizi si za kufanyia starehe bali ni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya wananchi wa Nyamazobe ambao anawapenda sana”. Amesema Waziri Jafo.