Katika kuadhimisha miaka 18 ya utoaji huduma kwa wateja wao Vodacom Tanzania (PLC) yafanya mwezi mzima wa October kuwa mwezi wa huduma kwa wateja. Vodacom, imeendeleza sherehe za wiki ya huduma kwa wateja, ambazo huadhimishwa wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka, na mwaka huu kauli mbiu ikiwa ni ‘Kusherehekea ubora wa utoaji huduma’.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Bi. Harriet Lwakatare, amebainisha kuwa, lengo kuu la kuendeleza maadhimisho hayo ni kuwashukuru wateja wao, watoa huduma na kuonyesha huduma mbalimbali wanazozindua kwa dhumuni la kuwasaidia wateja.
“Tunafurahia kuona Vodacom inaongoza katika kubadilisha maisha ya Watanzania zaidi ya milioni 12 na kuwaunganisha popote duniani. Huduma zetu zimekuwa za kwanza nchini, zimepokelewa vizuri na kuendelea kutufanya Mtandao bora wa simu nchini.”
Akiongelea mchango wa huduma zao kwa watanzania na uchumi kwa ujumla, Harriet alisema kuwa “M-Pesa imekuwa msaada mkubwa kwa huduma za kifedha kama kutuma na kupokea fedha ndani na nje ya nchi, kufanya manunuzi, na kulipa bidhaa na ankara”. Huduma nyongeza kama M-Pawa imesaidia kuboresha maisha ya watu daraja la chini na hata wa kati kwa kutoa mikopo isiyo na usumbufu kwa riba nafuu.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mageuzi yanayoongeza ubora wa huduma, kiongozi huyo anasema kazi yao hukamilika pale wanapohakikisha changamoto au tatizo la mteja limetatuliwa na si hivyo tu, bali na mteja amekiri kuridhika na utatuzi huo.
Vodacom, ijulikanayo kama ‘mtandao supa’ inajivunia kuwaunganisha ndugu, jamaa na marafiki kuwa na mtandao uliosambaa nchi nzima na kutoa intaneti yenye kasi zaidi. “Tunamfikiria mteja wetu na kumfanya kuwa kiini cha kila ubunifu tunaouzindua. Hatuishii hapo tu bali, tunaendelea kusikiliza na kuchukua maoni ya wateja wetu kwa ajili ya maboresho zaidi”.
Kuhusu kauli mbiu ya mtandao huo, ‘Yajayo Yanafurahisha’ Lwakatare amesema kwamba, kauli hii imelenga kuonyesha Vodacom imejidhatiti kuboresha huduma kwa wateja wao kupitia njia za kidigitali zaidi ambazo wateja wanapata msaada wa papo kwa hapo kwa kuchati moja kwa moja (Live chat) na watoa huduma.
Kadhalika, Lwakatare anabainisha kuwa kupitia mitandao ya kijamii Facebook, Instagram, na Twitter wana kitengo maalum chenye ueledi wa kutosha kumsaidia mteja kupata taarifa na ufumbuzi wa matatizo mbalimbali kwa haraka. Pia kupitia maoni yanayotolewa wakati wateja wanapakuwa application zetu kwenye ‘Google play’ au ‘App Store’, Vodacom imehakikisha maoni yao yanafanyiwa kazi na kupatiwa majibu papo hapo.
Lwakatare pia amethibitisha Vodacom inaendelea kusogeza zaidi huduma kwa wateja kupitia maduka yao yaliyo zaidi ya 400 nchini.
Kuhusiana na kutoa elimu kwa wateja kuhusu wimbi la matapeli ambao hutumia fursa ya M-Pesa kuibia wateja fedha, Harriet anasema Vodacom kwa sasa ina kampeni mahususi ya kuelimisha wateja.
Mara kwa mara, watumiaji wa simu za mkononi wamekuwa wakilalamika kupokea ujumbe mfupi wa maneno au kupigiwa simu wakielezwa kuwa wameshinda, kabla ya kupewa zawadi matapeli hao huwataka watume kiasi fulani cha pesa.
Watumiaji wa simu wanatakiwa kuwa makini pindi wanapopigiwa simu hasa na watu wasiowafahamu na pia kulinda na kutokutoa namba ya siri wala taarifa zinazohusu akaunti za fedha zao kwa mtu mwingine. “Tunapenda kuwajulisha wateja kuwa namba yetu inayotumika kuwasiliana na wateja wanaoshinda promosheni zetu au wanaohitajika kwa namna yoyote, huwa ni namba 0754 100 100 na si vinginevyo,” Harriet anabainisha.
Kuhusiana na namna Vodacom ilivyoboresha usalama wa mteja katika utumiaji wa huduma ya M-Pesa, Lwakatare amethibitisha usalama wa miamala ya wateja wao na kuwahakikishia wateja wao kuwa M-Pesa imethibitishwa na kampuni ya kimataifa ya GSMA kwa usalama wake na hudumu bora zaidi.
Changamoto nyingine inayoripotiwa na wateja ni miamala inayotumwa kimakosa, na Lwakatare amebainisha uwezekano wa wateja kuweza kurudisha miamala inayotumwa kimakosa punde wanapogundua wamekamilisha muamala usio sahihi.
Vodacom inaendelea kuboresha huduma kwa kuzindua mifumo ya kulipia bidhaa kwenye mitandao kama Amazoni, Ebay, Easybuy kidigitali kwa kutumia M-Pesa Mastercard ikiwa ni mpango wa kuhakikisha huduma zao zinawagusa watu katika sekta zote. Mkurugenzi huyo amemaliza mwezi huu kwa kuwashukuru wateja wao na kuwataka waendelee kutumia mtandao huo kwani hakika, yajayo, yanafurahisha!