Mkuu wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora Gift Msuya amewataka wananchi kufika wilayani humo na kutumia fursa ya uwepo wa maeneo makubwa ya uwekezaji na kueleza kuwa wanahitaji wawekezaji katika sekta mbalimbali kama benki, vituo vya mafuta, vituo vya mabasi na maeneo mengine mengi ya utoaji huduma.
“Tunahamasisha watu wengi waje kuwekeza kwenye maeneo hayo kwa sababu huduma nyingi za kimsingi tunazipata Tabora Manispaa kwa sasa. Mpaka sasa Halmashauri yetu haina hata kituo kimoja cha mafuta, haina maduka, haina hoteli kwa hiyo ni hitaji kubwa ambalo tunafikiri ni muhimu sana kwa ajili ya huduma kwa wananchi wetu. Lakini pia tunahitaji uwekezaji kwenye kiwanda cha kusindika ngozi, tuna wafugaji wengi na ngozi nyingi huwa wafugaji wakishapeleka pale ng’ombe zikichinjwa na kuuzwa ngozi huwa zikitupwa. Kwa hiyo tunahitaji kiwanda cha kuiongezea thamani ngozi na bidhaa za ngozi”. Amefafanua Mkuu huyo wa mkoa.
Msuya ameeleza kuwa baadhi ya kata kama Goweko, Sikizya, Kigwa, Bukumbi, Miyenze na Loya tayari zimeshatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wakati huo huo, yapo maeneo yaliyotengwa maalum kwa ajili ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.