Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda ametoa wito kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanza mchakato wa kuwekeza katika ubunifu wa teknolojia za kisasa na kuzalisha mashine za kurahisisha shughuli za viwanda nchini. Waziri Kakunda amesema hayo alipotembelea banda VETA katika maonyesho ya tatu ya bidhaa za viwanda Tanzania yaliyofanyika viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere, Sabasaba jijini Dar es salaam.
Waziri huyo amesema kufuatia dhamira ya serikali kwenda katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda, VETA inawajibu wa kuzalisha nguvu kazi yenye uwezo wa kubuni teknolojia ambazo zitarahisisha uchakataji wa malighafi zinazolishwa nchini. Kakunda amesema kuwa malighafi zikichakatwa ndani, zitasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo kusaidia wakulima kunufaika na kilimo wanachofanya.
“VETA mna nafasi kubwa nchini katika maendeleo ya viwanda na serikali inawategemea katika uzalishaji wa teknolojia na nguvu kazi ili kusaidia kusukuma maendeleo hayo,” alisema”. Amesema Waziri Kakunda.