Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu) Jenista Mhagama amesema hadi sasa, ofisi hiyo chini ya Baraza la Taifa la Biashara kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji, imefanikiwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji katika mikoa ya Kigoma na Dodoma kwa gharama ya Sh. 16 bilioni. Mradi huo ambao utekelezaji wake unajikita katika uwekezaji na biashara kwenye halmashauri kupitia mfuko wa SIFF, kuimarisha minyororo ya thamani na vilevile kuimarisha majadiliano baina ya serikali na sekta binafsi, tayari umeboresha mazingira ya biashara kwa wakulima na wavuvi mkoani Kigoma.
Waziri Mhagama ameeleza kuwa Baraza la taifa la biashara kwa ushirikiano na mradi huo wameweza kuwainua wananchi kiuchumi kupitia uwekezaji kwenye miradi midogo midogo ambayo imepelekea ongezeko la ajira na kipato.
“Nimetembelea mwalo na soko la samaki la Kibirizi, hapa mkoani Kigoma nimeridhishwa jinsi mradi huu ulivyoboresha miundombinu ya mwalo huu katika kuhakikisha wavuvi wanapunguza upotevu wa mazao ya samaki na dagaa. Niyaombe mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya yaendelee na mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha walengwa wa mradi huu wanaendelea kunufaika” Amesisitiza Waziri Mhagama.
Aidha, akiwa katika ziara hiyo, Waziri huyo pia ametembelea Kituo cha Biashara (One Stop Business Centre – Kigoma), soko la jioni la Mwanga, pamoja na mradi wa kuwezesha vijana kushiriki katika kilimo biashara na mnada wa mifugo Buhigwe.