Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge ametoa wito kwa watendaji mkoani humo kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kutengeneza mazingira rafiki ya biashara. Dk. Mahenge amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku moja cha Baraza la biashara mkoa wa Dodoma kilichojikita katika kujadili mwongozo wa uwekezaji mkoani humo. Dk. Mahenge amewaagiza watendaji hao kuzingatia weledi na tija ili kuwavutia wawekezaji kuwekeza mkoani humo kwa kuzingatia kuwa Dodoma ndiyo makao makuu ya nchi.
“Lazima utendaji wetu uwe wa namna bora na upekee katika kuweza kuvutia wawekezaji kwa kuwa na miundombinu rafiki ya biashara na kutatua changamoto zozote zinazoweza kuwakwamisha wawekezaji”. Amesema mkuu huyo wa mkoa.
Mbali na hayo, ameeleza kuwa, halmashauri zote zinatakiwa kuona umuhimu wa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutumia fursa zilizopo katika kufikia malengo ya kujenga uchumi endelevu.
“Ni vyema sasa kila halmashauri ikaona fursa na kuzitumia ikiwemo zile za kifedha na kuhusisha taasisi za kifedha ikiwemo mabenki ili kuona kila lengo linafikiwa na kuwa na uwekezaji wenye tija nchini”. Amesisitiza Dk. Mahenge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema ni muhimu kuzitumia fursa zilizopo jijini humo na kuwa na uwekezaji wenye tija kwa kila eneo kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
“Lazima fursa zilizopo Dodoma zitumike kwa malengo yenye tija kwa kuhakikisha mkoa unabaki kuwa kivutio cha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi”. Amesema Kunambi.