Baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha mabasi cha Ubungo jijini Dar es salaam, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaac Kamwelwe amebaini kupandishwa kwa nauli na madalali licha ya jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kuonya kupandisha bei za nauli kuelekea sikukuu za krismasi na mwaka mpya.
Mbali na nauli kupandishwa, imegundulika kuwa abiria wanaosafiri kuelekea mikoa ya Singida, Shinyanga, Tabora, Mbeya na Kilimanjaro, wamekumbwa na changamoto ya usafiri kufuatia wingi wa abiria na uchache wa mabasi hayo.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Waziri Kamwelwe amewaeleza waandishi wa habari kuwa abiria wanapandishiwa nauli hali inayowafanya kulipa zaidi ya nauli iliyopangwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
“Nimefika kituoni hapa saa 11:15 alfajiri na kuzunguka kwenye baadhi ya mabasi nikabaini kuwa baadhi ya abiria wanalipishwa nauli tofauti na bei elekezi ya serikali”. Amesema Kamwelwe.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ramadhan Kailima ametoa wito kwa abiria kutoa taarifa wanapokuta nauli zimepandishwa ili wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua. Naye Meneja wa kituo hicho, Imani Kasagala, amesema chanzo cha kupandishwa nauli kiholela ni baadhi ya wamiliki kupaki nje ya kituo na kutafuta madalali badala ya kuingia ndani ya kituo kama utaratibu unavyoelekeza.