Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini Tanzania (SAGCOT) Geoffrey Kirenga amesema kituo hicho kimejipanga kuchangia kuleta mageuzi makubwa ya kilimo hapa nchini ili kufanikisha uchumi wa viwanda. Kirenga amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam na kueleza kuwa, SAGCOT itaunganisha ngvu kutoka sekta binafsi na zile za umma ili kuchangia maendeleo na ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ujumla.
“Kama wadau katika sekta ya kilimo, tutashirikiana na serikali pamoja na wadau katika sekta binafsi kufanikisha azma ya serikali ya Rais Magufuli kuleta mageuzi makubwa katika kilimo, ili kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda. Ni ukweli usiopingika kuwa azma ya serikali ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025 itafikiwa kwa urahisi endapo uzalishaji na tija zaidi itapatikana katika sekta ya kilimo. SAGCOT ina imani kubwa na hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuwa zitazaa matunda”. Amefafanua Ofisa huyo.
Mbali na hayo, Kirenga pia amezungumzia ziara za Naibu Waziri wa Kilimo katika taasisi yake na kusema hatua hiyo inaashiria dhamira ya serikali kushirikiana na wadau wote kuboresha sekta ya kilimo.