Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge ameagiza uongozi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kupanga mikakati ya kumaliza changamoto ya msongamano hususani katika barabara ya kuelekea Dar es salaam. Dk. Mahenge ametoa agizo hilo wakati akikagua miundombinu ya barabara zinazozunguka jiji hilo ikiwemo ujenzi wa barabara ya Emaus-African Dream, barabara ya Martin Luther-Swaswa awamu ya pili pamoja na uboreshaji wa barabara za mjini kati.
Dk. Mahenge amesema wakati wakisubiri utekelezaji wa barabara hizo, wafanye mchakato wa kupunguza msongamano ndani ya Manispaa ya Dodoma kwani imekuwa kero katika barabara ya kisasa kwenda Morogoro hadi Dar es salaam.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi amewataka wananchi ambao wataathirika na ujenzi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika maeneo yao kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na kuwahakikishia usalama ili watekeleze majukumu yao kirahisi.