Home VIWANDAMIUNDOMBINU Sekta ya ujenzi yachangia asilimia 14 pato la taifa

Sekta ya ujenzi yachangia asilimia 14 pato la taifa

0 comment 86 views

Sekta ya Ujenzi imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Haya yamebainishwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Bungeni Jijini Dodoma

Amesema wastani wa mchango wa Sekta katika Pato la Taifa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2012 hadi 2022 ni asilimia 14.

“Serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa na makandarasi kutoka ndani na nje ya nchi,“ ameeleza Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amebainisha vipaumbele tisa vya Wizara ya Ujenzi itakavyotekeleza katika bajeti mwaka 2024/25.

Ameeleza kuwa bajeti itazingatia kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja iliyoharibiwa na mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya.

Bashungwa amesema pia kuendelea na utekelezaji wa miradi inayoendelea ambayo ni pamoja ujenzi wa barabara za kimkakati zenye kufungua fursa za kiuchumi na miradi ya kupunguza msongamano katika miji mikubwa kama vile Jiji la Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma.

Ameeleza ujenzi wa barabara zinazounganisha makao makuu ya mikoa, zinazounganisha na nchi jirani kwa kiwango cha lami pamoja na barabara za ulinzi, usanifu wa barabara mpya hasa mijini, miradi ya kimkakati ikiwemo kukamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege.

Nyingine ni mradi wa udhibiti wa uzito wa magari, ujenzi na ukarabati wa vivuko kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na miradi ya nyumba na majengo ya Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Bashungwa amesema kipaumbele kingine ni kuendelea na matengenezo ya barabara Kuu na za Mikoa kuhakikisha zinapitika majira yote ya mwaka na kuendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kwa lengo la kuongeza wataalam wabobezi wa ndani ili waweze kusimamia miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini.

Amesema pia kufanya mapitio ya Sera ya Ujenzi (2003) na Sera ya Taifa ya Usalama Barabarani (2009) pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali inayohusiana na Sekta ya Ujenzi ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na tabianchi.

Pia kuendelea kuimarisha mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi, kutumia teknolojia za gharama nafuu katika ujenzi wa barabara hususan katika maeneo korofi na kutekeleza Mkakati wa Uimarishaji wa Utendaji kazi wa TEMESA.

“Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi inayolenga kuondoa kero ya msongamano wa magari katika majiji.

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa upanuzi wa barabara ya Mwanza-Usagara-Daraja la JPM kuwa njia 4 (km 37): Sehemu ya Mwanza – Usagara (km 22),” ameeleza Bashungwa.

ameeleza miradi mingine kuwa ni mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya tatu ambao unahusisha barabara ya Nyerere kuanzia makutano ya barabara ya Kivukoni na Mtaa wa Azikiwe hadi Gongolamboto wenye kilomita 23.33.

Bashungwa amesema pia mradi wa BRT awamu ya 4 (km 30.12) utakaohusisha barabara ya Ali Hassan Mwinyi- Morocco- Mwenge – Tegeta; na kipande cha Mwenge hadi Ubungo.

Amesema pia ujenzi wa BRT Awamu ya 5 (km 27.6) ambao unahusisha barabara ya Mandela kuanzia makutano ya Ubungo- Bandari, makutano ya Mandela/Tabata- Tabata Segerea na Tabata- Kigogo.

Pia upanuzi wa barabara ya Mbagala Rangitatu kwend Kongowe (km 3.8) na daraja la Mzinga na upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki (km 11.6).

Amesema pia upanuzi wa barabara ya Uyole-Ifisi- Songwe Airport jijini Mbeya yenye urefu wa kilometa 36 kutoka njia mbili kuwa njia nne.

“Pia ukamilishaji wa ujenzi wa barabara ya mzunguko katika Jiji la Dodoma unaohusisha ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya mzunguko wa nje yenye jumla ya urefu wa kilometa 112.92 na ujenzi wa barabara hapa Dodoma ya mzunguko wa ndani (km 6.3),” amesema katika hotuba yake.

Bashungwa amesema pia ujenzi wa barabara ya mzunguko wa kati Dodoma (km 47.2), upanuzi wa barabara ya Dodoma – Morogoro eneo la Bunge hadi Mji wa Serikali Mtumba.

Pia ujenzi wa barabara za mchepuo za Singida (km 46), Iringa (km 7), Kilimanjaro na Songea (km14.4).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter