Home BIASHARA Vitu vya kujifunza kwenye biashara iliyofeli

Vitu vya kujifunza kwenye biashara iliyofeli

0 comment 115 views

IMEANDIKWA NA MAUREEN MURORI NA KUTAFSIRIWA NA LEAH NYUDIKE.

Kufeli kwa biashara sio mwisho, bali inaweza kuwa ndio mwanzo wa mafanikio katika safari yako ya kibiashara. Watu wengi waliofanikiwa duniani wamepitia changamoto ya kufeli mara nyingi kuliko unavoweza kuhesabu. Lakini kitu kimoja kinawafanya wafanane; ni maamuzi yao ya kuendelea kujaribu bila kukata tamaa.

Mara nyingi kushindwa kitu kunaumiza lakini ndivyo maisha yalivyo. Watu waliofanikiwa hutumia changamoto kujifunza jambo ambalo linawafanya wafike mbali.

Cheptiony Mutai, mjasiriamali kutoka Kenya amepitia changamoto nyingi zilizompelekea kushindwa katika ujasiriamali wake. Huku watu wengi wangefunga ofisi zao na kwenda nyumbani, Mutai ameamua kutumia changamoto hizo kama nyenzo pale atakapofungua tena ofisi.

Hivyo ameamua kuelezea mambo kadhaa ambayo unaweza kutumia ili kuboresha biashara yako.

Mwaka 2009, kabla ya kumaliza chuo Mutai alikuwa tayari ana kampuni inayohusu mambo ya burudani huko mjini Nairobi ambapo alikuwa akiwafanyia production wasanii wanaochipukia kutoka Olenguruone iliyopo kusini mwa Rift kaunti ya Nakuru ambako alikuwa anatokea. Alikuwa anafanya michakato ili wanamuziki hao waeze kutumbuiza mjini. Hii iliwasaidia kujulikana na kujipatia mashabiki, biashara ilikuwa ikiendelea vizuri.

Baada ya muda, Mutai aligundua kuwa wateja wake walikuwa na furaha lakini biashara yake haikuwa ikifanya vizuri. Kufanya kazi na wasanii unaojuana nao inamaanisha mnafanya kazi kwanza malipo baadae. Ambapo wengine walilipa na wengine walitokomea kusikojulikana bila kulipa. Baada ya muda akawa ana wasanii wengi bila mtaji wa kuendesha biashara hiyo.

Mwaka 2012 akabadilisha studio ya muziki kuwa kampuni inayojihusisha na mambo ya filamu na picha. Kwa bahati nzuri mwaka wa kwanza alifanikiwa kupata mkataba wa mwaka wa kufanya filamu za maandishi na picha. Biashara ilikuwa inaendelea vizuri hadi ilipoacha.

Rekebisha kosa pale tu unapolitambua

“Biashara yangu haikufa ndani ya siku moja”. Anasema Mtui

Anasema kulikuwa na viashiria vingi vilivyokuwa vikimuelezea kuwa mambo hayako sawa kwa muda mrefu lakini alikuwa akipuuzia.

“Niliendelea kufanya mambo ya filamu kwa zaidi ya miaka sita hadi biashara ilipokuwa haiendi kokote”. Anaongeza kusema.

“Sikuwa na wateja wapya, na wateja wangu wa zamani wakaanza kuondoka”.

Mabadiliko yalitakiwa kufanyika lakini hakuna mtu aliyefanya hivyo. Biashara yake ilivyokuwa ikiendelea kukua, Mutai aligundua kuwa anahitaji wasaidizi ili operesheni za biashara ziweze kwenda, hivyo akatafuta watu watatu ambao wana ujuzi wa kitekinolojia kuliko yeye. Kosa la kwanza alilolifanya Mutai lilikuwa ni kuajiri watu sio kwa sababu wana ujuzi unaotakiwa  au wana mapenzi na kazi hiyo bali kuajiri watu kutokana na mapendekezo ya marafiki na familia.

Baada ya muda aligundua tatizo hilo, lakini kwa kuhofia maneno ya marafiki na wanafamilia waliowapendekeza  wafanyakazi hao alliamua kuendelea kufanya nao kazi kwa matumaini kwamba watajifunza kadri ya muda. Pia Mutai alikiri kutowapa mafunzo wafanyakazi wake kufanya kazi bila kusimamiwa, hali iliyosababisha yeye kuwa anatafuta kazi za kufanya na hata wakizipata kazi hizo walikuwa na mchango mdogo kutokana na kutokuwa na ujuzi stahiki. Alivyoamua kuwaachisha kazi, biashara ilikuwa imeshakufa na hivyo akashindwa kujilipa na kuwalipa wafanyakazi hao.

Pata nyaraka stahiki

Serikali nyingi duniani humtaka mfanyabiashara kujisajili na kulipa kodi kama sheria inavyoeleza. Biashara inahitaji leseni sahihi ili iweze kufanya operesheni zake kwa uhuru. Kosa la pili lililosababisha biashara ya Mtui kurudi nyuma, ni ukosefu wa nyaraka stahiki. Anasema kuwa kutokana na suala hili makampuni makubwa yalikuwa yanaona hayupo tayari kwa ajili ya kazi na alishindwa kufanya kazi na serikali hivyo kupelekea kudorora kwa biashara.

“Nilikosa kibali cha biashara. Kutokana na hilo nilikosa tenda za serikalini na makampuni makubwa”

Kuwa na utaratibu wa kujiwekea kumbukumbu za kifedha

Ukiachana na kuwa na nyaraka stahiki, biashara inatakiwa kuwa na utaratibu wa kutunza kumbukumbu hasa za kifedha. Hii ni nyenzo kwa mfanyabiashara hasa katika kujua kama biashara haifanyi vizuri na hivyo kutafuta namna ya kurekebisha hali hiyo.

Katika kesi ya Mutai, utaratibu huo ungemuwezesha kujua kuwa biashara inafeli na hivyo hayupo katika hali ya kubadilisha biashara kama alivyofanya. Ukiachana na kuendelea kuwa na wafanyakazi hata kama biashara hairuhusu Mtui alifanya maamuzi mabaya zaidi kwa kuikopa biashara ili aweze kuwekeza katika kilimo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter