Home VIWANDANISHATI Rukwa yamkataa mkandarasi REA

Rukwa yamkataa mkandarasi REA

0 comment 98 views

Kufuatia kushindwa kufikia hata nusu ya utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) mkoani Rukwa, Mkuu wa mkoa huo, Joachim Wangabo amesema mkandarasi Nakuroi Investment amekataliwa kuendelea na mradi huo. Wangabo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa mkataba, mkandarasi huyo alitakiwa kutekeleza mradi huo katika vijiji 111 mkoani humo tangu mwezi Novemba mwaka 2017 lakini hadi Februari 2019, amekamilisha mradi katika vijiji 23 pekee.

“Itakapofika mwezi Juni huenda hata robo tutakuwa hatujafika, kwa hali hii niseme tu wazi huyu Mkandarasi Nakuroi Investment mimi naona uwezo wake ni mdogo lakini pia eneo amepewa ni kubwa sana huyu anashughulikia mkoa mzima vijiji tulivyonavyo ni 339 mkoani kwetu, hapa ni lazima Wizara ifanye kitu, mi niseme tu wazi kuwa ikifika mwisho wa mkataba wake hatutamkubali tena kuendelea na mkataba mwingine, watuongezee wakandarasi, tunahitaji kupata umeme katika vijiji vyetu vyote kwa mujibu wa mkataba”. Amesema Mkuu huyo wa mkoa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Rukwa, Gilles Daniel amesema changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ndio sababu ya kusuasua kwa mradi. Meneja huyo amedai changamoto kubwa imekuwa ni upatikanaji wa vifaa, kufuatia uzalishaji wake viwandani kuwa mdogo.

“Umeme umewashwa katika vijiji 23 tu peke yake, ni kweli kwamba mradi unasuasua hatujaenda kwa kasi ile ambayo inatakiwa kwa sababu ya changamoto nyingi ambazo zimetokea zinazosababisha mradi kusuasua lakini ni juzi tu Waziri alitoa maagizo ya kuwashwa vijiji vitatu kwa kila wilaya na utekelezaji umeanza na ndani ya siku mbili umeme utakuwa umewashwa ndani ya vijiji vitatu kila wilaya”. Amesema Kaimu huyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter