Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kahama, Anderson Msumba ametoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kama ambavyo taratibu zinavyoelekeza ili kuchochea maendeleo. Msumba amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambayo pia ametolea ufafanuzi suala la baadhi ya maduka kufungwa mjini humo. Akieleza kuhusu maduka hayo, Mkurugenzi huyo amedai tayari tume maalum imeshaundwa kufuatilia hali hiyo huku akikanusha taarifa kuwa Halmashauri imehusika kufunga biashara hizo.
“Ni kweli kuna baadhi ya wafanyabiashara wamefunga maduka, lakini hatujui kama wamefunga mitaji yao imeanguka au sababu tu wanataka kutoka kwenye leseni wapate kitambulisho ili wasilipe TRA? Tunalifanyia kazi, mtu ambaye hastahili tutahakikisha analipa kodi za TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania). Tusikimbie wajibu Kufunga biashara ili usilipe kodi si uzalendo, nadhani mwananchi ajivunie maendeleo ya nchi yake kwa kulipa kodi, wao tu wananchi watusimamie maendeleo pale ambapo wanalipa kodi na ili awe huru lazima atekeleze wajibu wake”. Ameeleza Msumba.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa ili kupata maendeleo ni lazima wananchi kulipa kodi kwani fedha hizo zinakwenda moja kwa moja kwenye miradi muhimu katika jamii kama vile elimu na huduma za afya.