Home FEDHA Wafanyabiashara, wamiliki majengo lipeni kodi kwa wakati-TRA

Wafanyabiashara, wamiliki majengo lipeni kodi kwa wakati-TRA

0 comment 151 views

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA Richard Kayombo amewataka wafanyabiashara pamoja na wamiliki wa majengo kulipa kodi kwa wakati, hasa kodi ya mapato awamu ya kwanza, kodi ya majengo na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Kayombo amewaambia walipakodi katika ofisi za TRA Vingunguti jijini Dar es salaam kwamba, kodi ya VAT inapaswa kulipwa hadi kufikia Machi 20 wakati muda wa kulipa kodi ya mapato ni hadi tarehe 30 Machi mwaka huu. Mkurugenzi huyo pia ameeleza kuwa mwisho wa kulipa kodi ya majengo ni Juni 2019.

“Ninachukua fursa hii kuwahimiza wafanyabiashara na wamiliki wa majengo mliopo hapa na wale watakaosikia taarifa hii kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuwahi kulipa kodi hizi kwa wakati ili kuepuka usumbufu na hatimaye kujikuta mnatozwa faini na riba. Tunaona serikali imepunguza kiwango cha kodi ya majengo, hivyo hakuna sababu ya watu kuchelewesha na kusubiri dakika za mwisho, tulifanye suala la ulipaji kodi kuwa utamaduni wetu kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Kayombo.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo ametoa tahadhari kuhusu uwepo wa watu wanaotumia jina la TRA kutapeli walipakodi wakidai kuwa ni maofisa wa mamlaka hiyo.

“TRA ina utaratibu wake wa kuwasiliana na wafanyabiashara na kuwajulisha siku rasmi ambazo maofisa wetu watakwenda kufanya ukaguzi na unafanyika kwa uwazi bila vitisho na si kwa taratibu nyinginezo”. Amesema Kayombo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter