Home BIASHARA Wafanyabiashara waja kivingine kuwanyonya wakulima

Wafanyabiashara waja kivingine kuwanyonya wakulima

0 comment 102 views

Wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, wamebuni namna mpya ya kuwaibia wakulima wa zao la vitunguu katika soko la kimataifa la Misuna lililopo Manispaa ya Singida. Mwenyekiti wa soko hilo, Abdalarahaman Mbogo, amesema kuwa wafanyabiashara hao wameanzisha tabia ya kuwafuata mashambani wakulima na kununua bidhaa hiyo kwenye magunia yanayojulikana kama Tshishimbi ambayo yamepigwa marufuku na uongozi kutokana na kuwa na ujazo wa kilo zaidi ya mia moja.

“Tunaomba serikali ya mkoa kushirikiana na wenzao wa vijijini na mikoa mingine inayolima zao hili kupiga vita magunia hayo ya nyavu yanayobeba vitunguu zaidi ya kilo 100”. Amesema Mbogo.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa magunia hayo yalipigwa marufuku na serikali kwa sababu yanamnyonya mkulima, ndiyo maana wafanyabiashara hao wanaamua kuwafuata mashambani wakulima hao ambapo hakuna utaratibu unaoeleweka wa kufanya mauzo. Ametaja njia nyingine ambayo si halali ni njia ya upimaji kwa kutumia ndoo kubwa.

“Pia kuna ujanja wa kutumia ndoo kubwa zinazotanuliwa kwa lengo la kumnyonya mkulima kule kule kijijini. Mbaya zaidi wanapopima kwa ndoo inabidi mpime ndoo sita ndipo eti wanahesabu gunia moja, jambo hili sio sawa, wanawanyonya wakulima”. Ameeleza Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Singida, Paskas Muragili amesema serikali ipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya wakulima huku akihimiza ushirikiano kati ya wakulima na serikali ili kutatua changamoto kama hizo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter