Home BIASHARAUWEKEZAJI Upanuzi hospitali ya Aga Khan kunufaisha wengi

Upanuzi hospitali ya Aga Khan kunufaisha wengi

0 comment 105 views

Hivi karibuni Hospitali ya Aga Khan, iliyopo jijini Dar es salaam ilisherehekea upanuzi wa hospitali hiyo ambao umegharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni 83.5, sawa na Bilioni 192 za kitanzania. Fedha hizo ni pamoja na mkopo wa muda mrefu wenye riba nafuu kutoka katika Shirika la Ufaransa (AFD) na ruzuku kutoka Mtandao wa Kimaendeleo wa Aga Khan (AKDN).

Binti Mfalme Zahra Aga Khan, mtoto wa Mtukufu Aga Khan alikuwepo katika uzinduzi huo kwa niaba ya baba yake, na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye aliongozana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Upanuzi wa hospitali hiyo umehusisha ongezeko la vitanda kutoka vitanda 70 hadi vitanda 170, jengo la hospitali kuongezwa ambapo hivi sasa hospitali ina kituo cha kutolea elimu ya matibabu. Pia upanuzi huo umehusisha vituo 35 nchini, huku vituo 23 kati ya hivyo vikiwa vimeshaanza kufanya kazi.

Huduma za Aga Khan Nchini Tanzania (AKHST) zilianza takribani miaka 90 iliyopita jijini Dar es salaam ambapo kwa upande wa afya, huduma hizo zimekuwa zikikua kwa kasi na kufanya hospitali ya Aga Khan kuwa na huduma za hali ya juu katika kanda. Kupitia Mtandao wa kimaendeleo wa Aga Khan ambao upo chini ya Mtukufu Aga Khan, wameweza kujenga vituo vya afya Uganda, Nairobi, Mombasa, na Kisumu nchini Kenya na kutoa huduma kwa wagonjwa zaidi ya 600,000.

Kupitia maboresho hayo katika msingi wa rasilimali na vituo vya mafunzo, hospitali ya AK Dar es salaam inatarajia kuboresha huduma za afya kama vile upatikanaji wa dawa za kutosha , huduma ya watoto na uzazi, maendeleo ya mipango mpya ya wataalamu katika cardiology, oncology na neurosciences. Hii itasaidia  kushughulikia ongezeko kubwa la vifo vinavyosababishwa na magonjwa ya muda mrefu, Tanzania na nchi nyingine barani Afrika.

Katika upanuzi wa awamu ya pili licha ya kuboresha miundombinu kama jengo la hospitali, vitanda, vyumba vya watoto na vyumba vya wakubwa upande wa tekinolojia pia umeboreshwa sana kwa mfano kuna uwepo wa teknolojia kama vile mifumo wa kumbukumbu na mawasiliano (PACS), mfumo wa taarifa za radiolojia (RIS), mfumo wa usafiri wa tubati za nyumatiki (pneumatic tubes transport system) na mifumo ya kompyuta ya ufuatiliaji wa wagonjwa pia imeanzishwa, lengo kuu likiwa ni kuboresha huduma hospitalini hapo.

Hospitali ya Aga Khan inatoa  huduma katika vituo vya matibabu ya msingi nchini kote, ikiwa ni pamoja na Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Mwanza, pamoja na Arusha. Kwa upande wa Dar es salaam kuna vituo sehemu mbalimbali kama Mbezi beach , kituo cha jiji, Masaki, Mikocheni na Tandika. Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki sehemu walipo.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter