Home VIWANDAMIUNDOMBINU Julai Tanzania kuzindua mpango wa uendelezaji miji

Julai Tanzania kuzindua mpango wa uendelezaji miji

0 comment 98 views

Uzinduzi wa mpango njia wa uendelezaji wa miji nchini (urbanisation road map) unatarajiwa kufanyika Julai mwaka huu baada ya kukamilika kwa uchambuaji wa maoni kutoka kwa wadau kuhusiana na mpango huo.

Hayo yameelezwa na Dk Lorah Madete, Mchumi Mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakati wa kufungua mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) katika ukumbi wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Mchumi Mwandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Lorah Madete akitoa neno la ufunguzi wakati wa mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF).

Alisema wakati taifa linatekeleza mipango yake ya maendeleo kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda, ni dhahiri kwamba suala la mipango miji ni lazima kutiliwa maanani.

Alisema kwamba miji yetu inatakiwa kukua kwa utaratibu ili kulingana na mahitaji ya uchumi wa viwanda.

Alisema kwa sasa kutokana na watu kutaka maisha bora wamekuwa wakitoka vijijini na kukimbilia mjini na hivyo kuleta shinikizo katika menejimenti ya miji.

Alisema kutokana na mazingira ya sasa katika miji yetu, ushiriki wa sekta binafsi katika kuboresha miji ni muhimu ili kukabiliana na kasi ya ukuaji wa miji.

Alitaka wataalamu wanaopitia mpango huo na kutoa maoni yao kuhakikisha kwamba wanawezesha Tanzania kuwa na miji inayokidhi mahitaji ya makazi; kwa kuwa miji iliyopangwa vyema ikifuata kanuni zote ikiwa ni pamoja kuwa na njia bora za kudhibiti uchafu, menejimenti na matumizi ya usafiri endelevu na kutumia nishati iliyo safi.

Bw. Anton Cartwright kutoka Taasisi ya Miji ya Afrika iliyopo Afrika Kusini, akielezea kilichojiri kwenye mpango wa taifa wa uratibu wa miji wakati wa mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF).

Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kuanzia mwaka 2017 kwa msaada wa Wizara ya misaada ya kimataifa ya Uingereza (DFID) na kwa ushirikiano na Wizara ya Fedha ya Tanzania walianzisha TUlab kwa lengo la kuangalia ukuaji wa miji endelevu, unaojali watu wake.

“Tunapoenda kwenye uchumi wa viwanda ni lazima tujiandae kwa uchipukaji na ukuaji wa miji, hivyo ni lazima tuingize mipango hiyo katika mpango huo mkubwa wa maendeleo kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda ‘Tanzania Development Vision 2025’ ” alisema Dk Madete.

Alisema wakati serikali kwa sasa inatekeleza awamu ya pili ya mpango wa maendeleo wenye lengo la kuweka msingi wa mapinduzi ya viwanda, ipo hatari kubwa kwamba Tanzania ipo katika hatari ya wananchi wake kutofaidika kiuchumi, kijamii na kimazingira kutokana na mlipuko wa ukuaji wa miji usiozingatia taratibu.

Hata hivyo alisema kwamba pamoja na kuwa na mpango wa ukuaji wa miji, mipango hiyo lazima iambatane na makubaliano ambayo taifa hili limetia saini ikiwamo Makubaliano ya Paris, Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, Ajenda Mpya ya Miji na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063.

Mikataba mingine ni ya Afrika Mashariki (EAC) 2050 na Jumuiya ya Ushirikiano ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC 2050.

Alisema kwamba ili kuwepo na mwenendo mzuri ni lazima wataalamu kuangalia namna ya kuendana na ukuaji wa miji ulio endelevu na salama na kujiongezea tija na ufanisi.

Bw Brent Cloete kutoka Afrika Kusini akiwasilisha utafiti unaolinganisha njia mbili za kiuchumi zilizochukuliwa na Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda wakati wa mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF) .

Alisema ni umuhimu huo ndio ulifanya Agosti 2017, Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na ESRF na taasisi ya Coalition for Urban Transitions (CUT) kuanzisha TULab ili kusaidia kuwa na mipango madhubuti ya maendeleo ya miji.

”Hatuwezi kufanikiwa bila uhusiano mzuri wa kiutendaji na hapo ndipo TULab inapoingia kusaidia mipango endelevu ya miji kwa kuwezesha jukwaa la majadiliano jinsi ya kuiendeleza miji yetu”

Awali akimkaribisha Dk Madete, Mkuu wa kitengo cha Uwezeshaji na Utawala Bora wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Danford Sango kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dk Tausi Kida alisema kwamba mkutano huo wa Saba ni muhimu kwani ndio wanaingia katika kipindi ushindani mkubwa wa kuweka sawa mawazo yatakayotumika kama ramani kuelekea miji yenye utaratibu.

Mkuu wa kitengo cha Uwezeshaji na Utawala Bora wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Danford Sango akitoa neno la ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk Tausi Kida wakati wa mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF) .

Alisema tangu kuanzishwa kwa TUlab Agosti 2017, imewezesha kufanyika kwa tafiti nne zenye lengo la kuangalia ukuaji wa miji na huduma zake. Aidha tafiti nyingine zilikuwa za kuona kinachokosekana katika uendelezaji wa miji na mahusiano kati ya serikali kuu na serikali za mitaa katika utoaji wa huduma kwa miji.

Tafiti hizo na nyingine zimewezesha kutengeneza mfumo wa maendeleo ya miji ambao bado unajaziwa nyama baada ya uzinduzi wa mazungumzo uliofanywa na Naibu katibu Mkuu, Menejimenti ya uchumi wa wizara ya fedha na Mipango Dk. Khatibu M. Kazungu, mjijini Dodoma hapo Novemba 28,2018.

Pamoja na kushukuru uwapo wa mkutano huo wa saba wa majadiliano, Dk Kida pia alishukuru Wizara ya Fedha na Mipango, Coalition for Urban Transitions (CUT), World Resource Institute (WRI) na African Centre for Cities (ACC) kwa kuwezesha mkutano huo.

Sehemu ya washiriki waliohudhuria mkutano wa saba wa Maabara ya Mipango Miji ( TULab) uliofanyika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Jamii na Uchumi (ESRF).

Alisema ni matumaini yake kwamba wataalamu watafikia muafaka wa kuwezesha taifa la Tanzania kuwa na ukuaji bora wa miji kuelekea uchumi wa viwanda na kipato cha kati.

“Naamini kwamba TULab ni jukwaa jema na salama ambalo linaweza kujadili na kuchambua masuala ya kila siku  ya ukuaji wa miji nchini Tanzania na kuja na hoja bora zaidi ya kuwezesha ukuaji wenye kukidhi matakwa ya wakazi” alisema Dk Kida katika hotuba iliyosomwa na Bw Sango.

Alisema pia TULab lengo lake ni kuangalia, kuchambua kwa undani juu ya sera za mipango miji na pia kuona changamoto za maendeleo na namna ya kukabiliana nayo.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter