Home BIASHARA Bidhaa bandia zinafikaje sokoni?

Bidhaa bandia zinafikaje sokoni?

0 comment 60 views

Kumekuwa na ongezeko kubwa la bidhaa bandia hapa nchini, jambo ambalo limekuwa likiwapa wasiwasi wananchi. Mamlaka husika zimekuwa zikifanya kazi kubwa kudhibiti tatizo hili kwa kuwa na wakaguzi kote nchini ili kupambana na wanaofanya vitendo hivi lakini bado wanaonekana kuzidiwa nguvu kwani bado tumeendelea kushuhudia bidhaa hizi zikiteketezwa kila siku.

Lakini kama mamlaka zipo kuchunguza na kuangalia ubora wa bidhaa ni vipi bidhaa hizi zinaingia mitaani? Wahusika wanazidiwa nguvu? Hadi sasa kuna waliochukuliwa hatua za kisheria? Wananchi nao wanatoa mchango gani kutatua suala hili?

Uwepo wa bidhaa hizi unahatarisha afya za wananchi ambao wengi wao wanashindwa kufahamu tofauti moja kwa moja, hali ambayo hupelekea mtu kununua bidhaa ambayo huenda ikasababisha matatizo ya kiafya. Mbali na hayo, uwepo na bidhaa bandia unasababisha hasara kwani mtu hutumia gharama kupata bidhaa fulani lakini baadae analazimika kuingia gharama nyingine tena ili kupata bidhaa hiyo hiyo yenye uhalali uliodhibitishwa.

Swali linakuja, baada ya mamlaka kukamata watu hawa wanaojihusisha na usambazaji wa bidhaa bandia, nini kinafuata? Hatua gani zinachukuliwa? Wanaadhibiwa kwa mujibu wa sheria? Mamlaka hizi zinachukua hatua gani kuhakikisha kuwa tatizo hili linapata suluhisho la kudumu? Wananchi wanaelimishwa vya kutosha kuhusu bidhaa bandia?

Uingizwaji wa bidhaa bandia unapaswa kudhibitiwa na kupewa kipaumbele zaidi. Ulinzi uimarishwe katika bandari, mipaka na viwanja vyote vya ndege. Hatua kali zaidi za kisheria zichukuliwe kwa wafanyabiashara pamoja na wote ambao kwa namna moja au nyingine wanachangia katika mtandao huo. Vilevile, TFDA pamoja na TBS wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ambazo unaweza kugundua bidhaa isiyo halali kabla ya kuinunua na kutumia. Vianzishwe vituo ambavyo vitakuwa vinapokea malalamiko au taarifa kutoka kwa wananchi ili kuzuia athari zaidi zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizi.

Wataalamu wanatakiwa kuhakikisha wanafanya ukaguzi mara kwa mara ili uwezekano wa wafanyabiashara kuweka sokoni bidhaa zisizofaa uwe mdogo. Washtukize zoezi hili mara kwa mara. Kufanya hivi kutapunguza tatizo hili na kuwaepusha wananchi na usumbufu wa aina yoyote kwa kiasi kikubwa. Tanzania bila bidhaa banda inawezekana. Wananchi wazidi kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha kuwa tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter