Home BIASHARA Wewe ni mfanyabiashara wa aina gani?

Wewe ni mfanyabiashara wa aina gani?

0 comment 123 views

Wafanyabiashara wengi wanapoanza biashara zao huwa wakarimu, nadhifu na wenye hamu kubwa ya kuwahudumia kwa umakini wateja wao. Kadri biashara inavyoendelea kukua, wengi huanza kufanya biashara kwa mazoea, jambo ambalo si zuri ukizingatia kuwa siku zote hakuna biashara isiyo na washindani.

Siku zote mfanyabiashara anapoanzisha biashara yake, huwa anatarajia mafanikio. Asilima kubwa hutegemea kuwa ndani ya muda mfupi maisha yao yatabadilika na kuwa mazuri zaidi. Changamoto hutokea pale ambapo mambo yanaenda tofauti na matarajio yake.

Ukweli ni kwamba kuna mengi ya kujifunza kabla ya kuanzisha biashara. Mojawapo ni mfanyabiashara kujiweka katika nafasi ya mteja wake. Je umewahi kuwaza kama wewe ungekuwa mteja, ungeweza kwenda kwenye biashara kama yako kupata huduma?

Kuna aina nyingi ya wafanyabiashara, Ukiachana na wale ambao hufanya shughuli zao kwa heshima, juhudi, uelewa na ustaarabu, aina tatu za wafanyabiashara hapo chini ndio kwa kiasi kikubwa wanapatikana katika jamii yetu.

Wafanyabiashara wengi wakiwa wameanza tu kupata mafanikio katika biashara zao huanza tabia za uongo bila kujua kuwa wanajiharibia majina yao. Kwa mfano, mteja anaipenda bidhaa mtandaoni na kuamua kuiagiza, mfanyabiashara anajua kabisa bidhaa hiyo ipo tofauti kwa macho lakini anaendelea kuchukua oda hiyo bila kumuelezea mteja tofauti iliyopo. Pale mteja anapokuja kupata bidhaa yake anabaki na manunguniko.

Kwa tabia kama hiyo, wewe kama mfanyabiashara unajiweka katika nafasi gani sokoni na machoni mwa wateja wanaokuamini? Unalenga kujinufaisha bila kujali kuwa unaonekana muongo? Unafikiri mteja huyo atatoa maoni gani kwa watu wengine kuhusu biashara yako? Siku zote, ni muhimu kuwa mkweli katika biashara ili wateja wako wafurahie huduma na wasipate wasiwasi utakaopelekea kufuata huduma hiyo kwa wafanyabiashara wengine.

Wapo wafanyabiashara ambao hutumia lugha mbovu kwa wateja wao. Kama mmiliki wa biashara, unapaswa kufahamu kuwa lugha ni muhimu. Je, wewe ungekuwa ni mteja unawasiliana na mfanyabiashara mwenye lugha mbovu ungejisikiaje? Ni lazima kutumia lugha nzuri kwa wateja na kuwa mkarimu. Hakuna mtu ambaye atafurahia huduma kama anayemuhudumia anakosa ustaarabu. Lugha mbovu hupelekea kukosa wateja na hivyo biashara kudorora.

Ni kweli kwamba kila mteja anatakiwa kununua bidhaa kulingana na fedha na bajeti yake lakini hii isikufanye wewe mfanyabiashara kuwa mbambikaji. Bei yako inatakiwa kulingana na bidhaa husika. Kama unaweka bei kubwa kwenye bidhaa za kawaida ni nani atanunua? Bila shaka utapata wateja lakini idadi haitakuwa kubwa kama ya mfanyabiashara ambaye hana tabia hizi. Ni muhimu wa kila mfanyabiashara kupata elimu kabla ya kuanzisha biashara ili kutambua athari zinazoweza kutokea na tabia kama hizi.

Wafanyabiashara wanatakiwa kuwa makini katika biashara zao, kwa sababu lengo la kufungua biashara ni kujipatia kipato. Ili kupata maendeleo ya kiuchumi, ni muhimu kuwa na misingi mizuri ambayo itawafanya wateja kukuamini na kufurahia huduma. Bila kufanya hivyo, unaiweka hatarini biashara hiyo ambayo inakuingizia fedha. Endelea kujifunza, kuwa mvumilivu na endesha shughuli zako kwa ukarimu.

Ukiachana na aina tatu nilizozitaja, kuna wafanyabiashara ambao wanastahili pongezi kwa sababu ya juhudi, ukarimu na heshima kubwa wanazozipa biashara zao. Wafanyabiashara wenye lugha nzuri, wenye kusaidia wateja kufanya maamuzi mazuri, walio na mfumo ambao unasaidia wafanyakazi kufanya shughuli  zao inavyotakiwa ni mfano wa kuigwa.

Elimu na kujifunza katika biashara ni muhimu sana. Jifunze kutoka kwa wafanyabiashara wenzio ili uzidi kusonga mbele. Kuna wafanyabiashara si wachoyo wa maarifa na hao ndio wanafaa kwenye ulimwengu wa kiuchumi. Hata kama mnafanya shughuli moja, hawaoni shida kukufundisha ili wote kwa ujumla wenu mpate mafanikio.

Ukiachana na yote hayo, suala la muda ni muhimu kwa mfanyabiashara na mteja. Kuna wafanyabiashara ambao huhakikisha wanapeleka oda kwa mteja katika muda waliokubaliana. Kujali muda ni kipengele muhimu sana katika biashara hususani kwa mteja kwani huongeza uaminifu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter