Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga amesema ili watanzania waweze kupanga matumizi bora ya mikopo wanayopata, kuna umuhimu wa kupewa elimu ya fedha katika mfumo wa taarifa za mikopo. Gavana Luoga amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uelimishaji wa umma kuhusu taarifa za mikopo na fedha na kusisitiza kuwa elimu hiyo ni muhimu ili kuhakikisha mikopo inatumika vizuri.
“Kampeni hii ya elimu kwa umma inalenga kuwaelimisha watumiaji wa huduma za fedha na wadau wa wengine kukuza uelewa wao kuhusu taarifa za mikopo ili kuongeza ushiriki katika matumizi katika matumizi ya taarifa za mikopo hapa nchini”. Amesem Prof. Luoga.
Naye Meneja Msaidizi wa Mfumo wa Kumbukumbu za Wakopaji BoT, Nkanwa Magina amesema lengo la kampeni hiyo itakayofanyika kwa miezi mitatu ni kuongeza uelewa kwa wananchi, mwamko kuhusu taarifa za mikopo na vilevile kukuza upatikanaji wa mikopo.
“Kaulimbiu katika kampeni hiyo ni : “Pata taarifa yako ya mikopo leo. Angalia hali yako ya kifedha ili kupanga mustakabali wako bora wa kesho” inaungwa mkono na wadau mbalimbali katika sekta ya huduma za fedha. Wadau hao wameahidi kusaidia kusambaza ujumbe kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa mikopo na jinsi watanzania wanavyoweza kuishi maisha bora kwa kuweza kupata taarifa za mikopo yao na kujua historia ya mikopo yao”. Amesema Magina.