Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limefanya operesheni ya kushtukiza katika soko la krokoni, Arusha, na kubaini wafanyabiashara wanaendelea kuuza nguo za mitumba zilizopigwa marufuku na Serikali.
Ofisa Uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, amesema kuwa Shirika hilo limefanya operesheni hiyo ya kushtukiza ili kufuatilia kama wafanyabiashara hao wametii agizo la serikali. Andusimile ametaja baadhi ya nguo ambazo wamefanikiwa kuzikamata katika soko hilo kuwa ni taulo, nguo za kulalia, chupi, sidiria, na soksi.
“Sasa bidhaa hizi sisi tumezikamata na tunazipeleka kuziteketeza kwa gharama zetu sababu hawa wafanyabiashara wadogo hatuwatozi gharama za kuteketeza, ila wale wafanyabiashara wakubwa tukiwakamata na bidhaa hizi tunawatoza faini pia wanalipa gharama zote za kuteketeza” ameeleza Ofisa huyo.
Pia amewataka wafanyabiashara kufuata sheria na kanuni wanazoelekezwa ili kuepuka hasara na gharama zisizokuwa za muhimu.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa TBS Lucas Gwila, amesema wananchi na wafanyabiashara wanatakiwa kuachana na matumizi ya nguo hizo ili kuzilinda afya zao na madhara ya nguo hizo ikiwemo magonjwa ya ngozi.
“Sasa kilichofanyika baadhi yao sio waaminifu wanaendelea kuagiza na kuzipitisha njia za panya na matokeo yake yanawagharimu mfanyabiashara mdogo kama huyu na sisi tukikuta tunafuata sheria ya kuziondoa bidhaa hizo sokoni hata kama hatujamkuta mfanyabiashara mwenyewe katika bidhaa zake” amesema Gwila.