Home VIWANDANISHATI Mradi wa Stigler’s Gorge kuimarisha viwanda na utalii

Mradi wa Stigler’s Gorge kuimarisha viwanda na utalii

0 comment 148 views

 

Na Mwandishi wetu

Mradi mkubwa wa kufua umeme wa Stigler’s Gorge uliopo Mto Rufiji unatarajia kuanza muda wowote kuanza sasa. Inategemewa kuwa pindi utakapokamilika, utaongeza upatikanaji wa umeme na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa azma ya kubadilisha nchi yetu na kuifanya kuwa Tanzania ya Viwanda.

Wakati anatembelea mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Vedast Makota amesema kuwa mbali na upatikanaji wa umeme, tatizo la maji ambalo limekuwa kilio cha siku nyingi litatatuliwa kwani kupitia mradi huu maji yataongezeka.

NEMC pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wametembelea mradi huo ili kuangalia hatua gani zinapaswa kuchukuliwa kimazingira, pia kupata taarifa husika juu ya mradi huo. Yote hawa yakiwa katika kufanikisha nchi yetu kuwa inayotegemea viwanda katika kujiletea maendeleo.

Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mradi huu unakamilika hivi karibuni. Utekelezaji wa radi huu pia unategemewa kuimarisha sekta ya utalii katika maeneo hayo. Geoffrey Tengeneza, Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB) anaongeza kuwa mradi huu kwa upande wa utalii utasaidia kuimarisha usalama wa watalii na mali zao na kutatua kero kubwa ya maji ambayo yamekauka kabisa kwa sasa, hivyo kuongeza thamani na kupanua wigo katika shughuli za kitalii katika eneo hilo.

Kwa niaba ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, muwakilishi wao Gregorian Kalokola amesema kuwa kufuatia mradi huo mkubwa, taifa litanufaika kwa kiasi kikubwa na sekta za viwanda na utalii zitumie nafasi hii kujiletea maendeleo na kuongeza pato la taifa.

Mradi huo wa umeme utachukua asilimia tatu katika mbuga ya Selous na ukifanikiwa, utawezesha nchi kuzalisha megawati 2100 zitakazotumika katika uzalishaji viwandani.

Kwa muda mrefu sasa, eneo hilo ndio sehemu pekee inayofaa katika utalii wa picha na uwepo wa maji ya uhakika utapelekea watalii kuongezeka katika siku za usoni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter