Taarifa kutoka kampuni ya Tullow Oil ya Kenya imeeleza kuwa, nchi hiyo itaanza kuuza mafuta yasiyosafishwa kwenye soko la kimataifa kati ya Julai na Septemba mwaka huu. Baada ya uzinduzi rasmi wa uuzaji wa mafuta hayo, nchi hiyo itakuwa ya kwanza katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kufanya biashara hiyo kimataifa.
Kampuni ya Tullow Oil ambayo ni mashuhuri kwa utafutaji wa mafuta katika eneo la Turkana nchini humo inaeleza kuwa hadi sasa, mapipa takribani 10,000 yameshagunduliwa kutoka Lokichar hadi Mombasa.
Kufuatia ongezeko la mafuta kutoka Lokichar hadi Mombasa, mapipa ya mafuta yameongezeka kutoka 600 hadi 2000 kwa siku. Hata hivyo kampuni hiyo ilisitisha shughuli zake kutokana na mfarakano waliokuwa nao na serikali nchini humo kwa takribani miezi miwili, lakini baada ya makubaliano wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao ambapo imeelezwa kuwa mapipa 80,000 ya mafuta yameshasafirishwa Mombasa tayari kwa kusafirishwa sehemu mbalimbali.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Paul McDade amesema wanasubiri ruhusa kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta ambayo itawezesha kampuni hiyo kuongeza mapipa na kufika 2,000 kwa siku huku mzigo wa kwanza ukitarajiwa kusafirishwa nje ya nchi.