Naibu Waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege amesema bungeni Dodoma kuwa serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 260 kwa ajili ya kukarabati barabara zilizoharibika jijini Dar es salaam kutokana na sababu mbalimbali. Kandege amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Antropia Theonest aliyehoji kuhusu mkakati wa serikali katika kushughulikia changamoto ya ukosefu wa madaraja katika barabara za jimbo la Segerea.
“Serikali imesaini kandarasi ya Sh. 260 bilioni kukarabati barabara na miundombinu iliyoharibika jijini Dar es salaam ambako tayari kumefungwa taa 5,000 za barabarani”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Vilevile Mbunge huyo amehoji ni lini serikali itamaliza kero ya ukosefu wa madaraja katika jimbo hilo ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 15, na lini barabara ya Segerea Sheli kwenda Kipawa kupitia Seminari yenye urefu wa kilomita 2.93 itaanza kujengwa.
“Barabara hii inapita katika Mto Msimbazi ambako hakuna daraja changamoto iliyopo ni kutanuka kwa Mto huo hivyo kuhitaji ‘study’ (uchambuzi) ya kina na mapitio ya usanifu ili kupata mahitaji halisi ya ujenzi wa daraja hilo”. Amesema.