Zao la tikiti maji ni moja kati ya mazao maarufu zaidi ya biashara duniani kote. Matikiti maji ni jamii aina ya matunda au mbogaboga inayotambaa. Zao hili lina faida lukuki ukilinganisha na mazao mengine kwa muda mfupi. Katika shamba la ukubwa wa ekari moja, mkulima anaweza kuvuna kiasi cha tani 15-36.
Matikiti maji hustawi katika maeneo yenye joto la wastani ikimaanisha kuwa haihimili hali ya joto kali, baridi kali, mvua nyingi wala udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu. Matikiti hukua vizuri katika maeneo yenye joto la wastani (kati ya 21 – 30) na huchelewa kuota pale inapopandwa katika maeneo yenye joto chini ya nyuzi 15. Yanahitaji millimita 400 mpaka 600 za mvua kwa msimu na udongo wenye rutuba pamoja na virutubisho. Mara nyingi kipimo cha pH kinashauriwa kuwa kati ya 6.0 na 7.0 japokuwa mmea unaweza unaweza kustahimili udongo wenye pH 5.0/
Baadi ya mikoa ambayo kilimo hichi kinakubali vizuri hapa nchini ni Pwani, Dar es salaam, Mtwara, Morogoro, Tanga na Lindi. Msimu mzuri wa kuoanda matikiti ni kikupwe yaani mwezi wa tatu mpaka wa tisa.
Wakati unaandaa shamba kwa ajili ya matikiti maji, ni muhimu kufyeka vichaka na ng’oa visiki vyote. Kabla ya kupandikiza, udongo unapaswa kutifuliwa na majani kuondolewa. Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa.
Wakati wa upandaji, ni muhimu kuzingatia kuwa; katika shamba la ukubwa wa hekta moja, kilo 3 hadi 4 za mbegu zinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila shimo. Usipande katika kitalu kwa sababu miche yake ni dhaifu sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa mita 1 hadi 2 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 – 3 kutoka mstari hadi mstari.
Wakati unachagua mbegu kwa ajili ya tikiti maji, mbegu maarufu ya tikiti ni Sukari F1. Mbegu nyingine ni pamoja na Arashani F1 (Kutoka Syngenta), Sukari F1 (Kutoka East Africa Seeds), Sugar King F1 (Kutoka Africasia), Juliana F1 (Kutoka Kiboseed), Zebra F1 (Kutoka Balton) na Pato F1 (Kutoka Agrichem).
Katika kilimo hiki, shamba linatakiwa kumwagiliwa mara kwa mara hasa katika msimu wa jua kali. Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni kipindi cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya kuvuna. Ukosefu wa maji ya kutosha ni chanzo cha kutengenezwa kwa matunda ambayo sio mazuri.
Matikiti yanayochukua muda mfupi sana kukomaa. Kwa kawaida, huwa tayari kwa kuvuna baada ya siku 80 hadi 100 baada ya kupanda. Vuna wakati tunda limeiva kabisa. Vuna kwa wakati unaofaa. Hifadhi katika eneo lenye ubaridi wa nyuzi 15 hadi 20. Hifadhi vizuri, unyevua-anga (humidity) unatakiwa kuwa 80% hadi 85%. Mara tu baada ya mavuno, peleka matikiti yako shambani kwa ajili ya kuuza.