Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Adolf Ndunguru amesema serikali imefanya vizuri katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, uchumi, miundombinu pamoja na viwanda. Naibu huyo amesema hayo jijini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kufanya tathmini ya Ripoti ya utekelezaji wa malengo hayo yaliyosainiwa tangu Septemba 2015 na kuanza kutekelezwa Januari 2016.
Ndunguru amesema kuwa wadau kutoka sekta binafsi, asasi zisizo za kiraia, wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa (UN), Zanzibar pamoja na washirika wa maendeleo (DP) wamekutana kwa lengo la kutathmini, kutoa maoni na kuboresha ripoti hiyo kabla ya kuiwasilisha UN Mwezi Julai mwaka huu.
Katika maelezo yake, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema tangu mwaka 2016, serikali imeboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu kwa kufanya upanuzi na kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari (kidato cha nne). Aidha kwenye sekta ya afya, serikali imefanya maboresho kwa kujenga miundombinu ambayo imewezesha utoaji huduma pamoja na kuongeza bajeti ya Wizara hiyo.
“Serikali katika kuinua uchumi, imefanya vizuri katika kupunguza mfumuko wa bei ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo yaliyokusudiwa na Umoja wa Mataifa katika agenda ya 2030”. Amesema Ndunguru.