Kilimo cha parachichi kinaendelea kukua hasa katika nchi za Afrika Mashariki. Pia kilimo hichi hakihitaji fedha nyingi na subira ya ukuaji wa matunda haya mara nyingi huambatanishwa na faida kubwa wakati wa mavuno.
Kwa Tanzania, kilimo hichi kimeanza kushika kasi zaidi mwaka 2015 ambapo baadhi ya watu walijitokeza na kuelezea mafanikio waliyopata kutokana na kilimo cha parachichi. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012, kiasi cha mauzo ya nje ya parachichi la Tanzania ilikuwa ni kilo 488,492, miaka mitatu baadae mwaka 2015 Tanzania ilisafirisha Kilo 2,579,976, ikiwa ni ongezeko la 428.48%.
Nchi za Ulaya kama Denmark, Ufaransa, Uingereza, Norway na Uholanzi zimeonyesha kufurahishwa na maparachichi yanayotoka nchi za Afrika Mashariki hususani Tanzania. Mikoa iliyojikita zaidi na uzalishaji wa zao hili ni Kilimanjaro, Mbeya, Njombe na Iringa. Hii ni kutokana na hali ya hewa ya baridi iliyopo katika mikoa hiyo.
Wakulima wengi wanaojihusisha na kilimo hiki huuza katika soko la nje. Wengi wao wanalima zaidi aina ya parachichi inayoitwa Hass, kwa sababu parachichi hii ina sifa kubwa ya kukaa muda mrefu bila kuoza. Parachichi la aina hii hutambulika kwa muonekano wa ngozi yake ambayo huwa inakuwa na vipele.
Baadhi ya makampuni ambayo yamewanufaisha wakulima wadogo wa zao hili kwa kununua matunda hayo na kuyasafirisha nje ya nchi ni kampuni ya Africado iliyopo Kilimanjaro ambapo watu zaidi ya 2,000 wamenufaika na zao hilo kupitia kampuni hiyo. Licha ya kuuza zao hilo, watu waliopo karibu na kampuni ya Africado wamenufaika na ajira. Kampuni nyingine zinayofahamika kwa usafirishaji wa zao hili nje ya nchi ni kampuni ya Rungwe Avocado Limited na Cuser Africa Limited ambazo zote kwa kiasi kikubwa zimewanufaisha watanzania wanaojihusisha na kilimo cha parachichi.
Ni muhimu kwa serikali kuwezesha vijana nchini hasa wasio na kazi za kuajiriwa kujihusisha na kilimo hiki kwa kuwa hakina gharama hivyo kila mkoa wenye hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa zao hili ungekuwa na mchakato wa kuunda vikundi ambavyo vitatengewa bajeti kwa ajili ya kuchochea kilimo hicho na kuwainua vijana ili waweze kunufaika, kujikimu kimaisha na kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla
Ni muhimu kwa mkulima yoyote anayetaka kuanzisha kilimo hiki kuwa makini, kwa sababu baadhi ya wazalishaji wa miche ya maparachichi wamekuwa sio waaminifu hivyo unaweza kununua miche mingi na kupata hasara. Inashauriwa kuwasiliana na wataalamu wanaohusika na kilimo cha matunda ili kutengeneza mpango mzuri wa uzalishaji na mwisho wa siku kupata faida.