Biashara ya samaki kwa ujumla ina faida sana. Kuna watu wengi wamefanikiwa kupitia biashara hii kwa kuanza na mtaji mdogo. Jambo la muhimu kwa mtu yeyote anayetaka kuanzisha biashara hii ni kufanya utafiti wa kutosha ili kuepukana na matatizo mbalimbali.
Mambo haya yatakusaidia kufanya maamuzi sahihi kama unafikiria biashara ya ufugaji wa samaki
ENEO LA KUFUGIA
Kama inavyofahamika samaki hukua na kuishi ndani ya maji hivyo hakikisha unajua samaki wako utawafuga wapi, navilevile zingatia usalama wa eneo hilo. Unaweza kufuga samaki kwenye mabwawa ya kuchimba, au hata kwenye matenki yenye muundo wa bwawa ili mradi kuwe na uhakika wa upatikanaji wa maji na miundombinu itakayokuwa inahitajika kuwezesha ufugaji huo.
MTAJI
Baada ya kuwa na uhakika wa eneo, ni muhimu kwanza kufikiri kama unataka kufanya ufugaji mkubwa au mdogo. Inashauriwa kuanza kidogo kama unafanya ufugaji binafsi ili kujua kama utaweza kukabiliana na changamoto hususani za kifedha. Mtaji unaweza kupatikana kupitia akiba binafsi, mkopo benki au katika taasisi za kifedha, mkopo kutoka kwa ndugu na jamaa au unaweza kumshauri mtu awekeze fedha zake katika mtaji huo kwa makubaliano ya malipo kwa riba baada ya muda fulani.
ELIMU
Sio kila mtu aliyeanzisha mradi wa samaki amesomea mambo yanayohusu uvuvi, wapo watu wengi wameanzisha biashara ya kufuga samaki na wakafanikiwa kutokana na kujifunza kuhusu mradi huo kupitia vitabu na mitandao. Hivyo hakikisha unajua wapi utapata elimu ya kutosha kuhusu mradi wa samaki ili kupata matokeo mazuri. Unaweza kupata elimu kuhusu ufugaji wa samaki kutoka kwa wataalamu wa masuala ya uvuvi, kupitia vitabu pamoja na mitandao kama youtube n.k.
AINA YA SAMAKI
Ni muhimu kufanya maamuzi kuhusu aina ya samaki unaotaka kufuga. Kuna aina nyingi za samaki lakini wafugaji wengi wanapendelea kufuga samaki aina ya Sato/perege (tilapia) na Kambale (Catfish).
Inaelezwa kuwa aina hizo mbili ni rahisi kufuga kwa sababu upatikanaji wa chakula chao ni rahisi na hukua kwa wingi na kwa haraka zaidi pia nyama zao hupendelewa zaidi kutokana na ladha yake kuwa nzuri.
Aidha, unapaswa kujua ni wapi utapata vifaranga wa samaki na vilevile gharama zake. Kama utamtumia mtaalamu basi itakuwa rahisi kupata maelekezo yote ya msingi.
SOKO
Soko ni jambo la muhimu sana kwa sababu baada ya kukuza samaki wako inabidi wauzwe. Ni muhimu kujua wapi utawauzia samaki wako. Unaweza kutafuta masoko kwa wafanyabiashara wa samaki katika masoko ya kawaida na kutokana na utandawazi, unaweza kujipatia soko kwa kutangaza biashara yako kwenye mitandao ya kijamii. Hakikisha unazingatia usafi, na kwa sababu watu wanavutiwa zaidi na urahisi wa mambo, unaweza kuwa mbunifu kwenye biashara yako kwa kuwatengeneza samaki wako na kuwaweka katika vifungashio ambavyo vitamvutia mteja.
Zingatia Sheria na kanuni za biashara hii, ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza.