Soko ni kipengele muhimu kwenye sekta ya biashara na ili unachofanya kilete mafanikio mauzo yafanyike na faida ipatikane la sivyo mfanyabiashara atalazimika kufunga biashara. Wafanyabiashara wengi hufikia uamuzi huo kutokana na kushindwa kuweka mikakati ya kufanya utafiti wa soko la bidhaa wanazotaka kuuza, jambo ambalo linapelekea biashara kushindwa kumudu ushindani wa soko na hatimaye kufungwa.
Ifahamike kuwa hakuna biashara isiyo ya mshindani hivyo ni muhimu kwa mfanyabiashara kufanya utafiti wa soko ili kuwa na muelekeo utakaoleta matokeo mazuri. Mfanyabiashara anashauriwa kuangalia washindani wanaofanya vizuri, wanaofanya biashara inayoendana na ile anayotarajia kuianza na hata kutathmini kuhusu washindani watakaokuja baadae. Tathmini ya mambo hayo humsaidia mfanyabiashara kufanya maamuzi sahihi kwa ujumla.
Ukiwatambua washindani wako itakuwa rahisi kujua mapungufu yaliyopo na hivyo kurekebisha au kupunguza mapungufu hayo. Siku zote wateja huenda sehemu zinazovutia inaweza kuwa katika upande wa bei, eneo, huduma, bidhaa yenyewe n.k hivyo ni muhimu kuwa na uimara katika mambo kama hayo ili kuhakikisha mteja anavutiwa na biashara na bidhaa zako zinajipatia soko la uhakika.
Unaweza kuandaa jedwali lenye orodha ya washindani wako ukieleza vitu vinavyowavutia zaidi wateja wao huku ukilinganisha na mapungufu uliyonayo katika huduma au bidhaa unayofikiria kuanzisha.
Baada ya kutambua hayo ni muhimu kujiuliza mipango waliyonayo washindani wako katika kukabiliana na vitisho na fursa katika tasnia husika. Kuna masuala ya kiteknolojia, na utandawazi yanaweza kuathiri biashara hivyo unatakiwa kujua jinsi gani utaweza kukabiliana na vitishio vinavyoweza kutokea mbeleni na kuweza kuathiri biashara yako. Kwa mfano, kama unataka kuuza duka la vifaa vya simu, umejiandaaje hapo mbeleni kama kila mtu atakuwa anachaji simu bila kutumia chaji? Na unafikiri washindani wako wamejiandaaje ili kuendeleza biashara kulingana na mwenendo wa kasi ya ukuaji wa teknolojia?
Ikiwa unafahamu washindani wako, mapungufu uliyonayo, vitisho vilivyopo na fursa zilizopo katika biashara unayotaka kuanzisha sasa unaweza kufanya maamuzi ya aidha kuendelea na mchakato wako wa kuanzisha biashara husika au kutoendelea nayo na badala yake kufikiria shughuli nyingine.