Home BIASHARAUWEKEZAJI Maeneo kando ya SGR kuendelezwa

Maeneo kando ya SGR kuendelezwa

0 comment 109 views

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametembelea wananchi wa vijiji vya Kwala na Soga vilivyopo Kibaha mkoani Pwani ambapo vijiji hivyo ni kati ya maeneo ambayo mradi wa reli ya kisasa wa SGR unapita.

Wakati wa mazungumzo yake na wananchi wa vijiji hivyo, Waziri Lukuvi amesema kuwa serikali imedhamiria kuyapanga maeneo yote inakopita reli hiyo ili kuhakikisha shughuli zinazofanywa na wilaya na vijiji kando ya reli hiyo zinaendana na shughuli za kiuchumi za mradi huo.

Pia amewatoa hofu wananchi kuhusu kunyang’anywa maeneo wakati shughuli hiyo inaendelea na kufafanua kuwa, maeneo hayo yatapangwa kimji na kuainishwa matumizi yake ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda, hoteli na maduka makubwa. Waziri huyo amewataka wananchi kuwa na subira ikiwa wanataka kufanya uendelezaji mdogo.

“Wilaya na vijiji vyote reli ya SGR itapita ardhi yao itapangwa na wale wananchi walio kando ya reli itakapopita wasubiri wasiwe na wasiwasi ardhi ya maeneo yao itengenezwe mpango na muongozo kuhusiana na maeneo hayo utatolewa. Tukiacha maeneo ya kandokando ya reli bila kupangwa na kupima kutafanyika vitu vya ajabu, reli hii ina faida kubwa, hivyo lazima kupanga maeneo inakopita ili kwenda sambamba na shughuli za kiuchumi za maeneo hayo” ameeleza.

Pamoja na hayo, amesema fedha za kutekeleza mpango huo zimeshatengwa na wanapanga maeneo hayo ili kufanikisha mpango mzima wa uendelezaji wa ukanda wa kiuchumi katika maeneo husika ili ufahamike kitaifa na kimataifa ili kuwavutia wawekezaji watakaovutiwa kuwekeza katika maeneo hayo.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter